MBIO za kuwania Kiatu cha Dhahabu zitaendelea tena kesho wakati George Mpole atakaposhuka dimbani kuiongoza Geita Gold FC kuivaa Tanzania Prisons kwenye mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mpole ambaye ana mabao 14 sawa na Fiston Mayele wa Yanga, wanachuana vikali katika mbio hizo za kumaliza kinara wa mabao kwenye ligi hiyo ambayo inaelekea ukingoni kwa sasa.
Yanga inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 64, 13 zaidi ya Simba iliyopo nafasi ya pili, tayari timu hizo zimeshuka dimbani mara 26, huku kwa Geita mchezo huo wa kesho ukiwa ndio wa 26 kwao.
Hivyo, kama Mpole atafunga kesho dhidi ya Tanzania Prisons inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani, atakuwa ameweka pengo kubwa kwa Mayele kwani tayari atakuwa mbele kwa mabao wakati timu zao zikiwa zimecheza mechi sawa.
Katika mbio hizo, wawili hao wanafuatiwa kwa karibu na Riliants Lusajo wa Namungo ambaye hadi sasa amecheka na nyavu mara 10, akifuatiwa na Abdul Sopu wa Coastal Union mwenye mabao tisa, huku Rogers Kola wa Azam FC akiwa na mabao nane nyuma yake.
Straika wa Simba, ambaye ametwaa kiatu hicho kwa misimu miwili akiwa na Wekundu wa Msimbazi hao, msimu huu ameshindwa kuonyesha makeke yake ya kucheka na nyavu kwani ana mabao saba tu sawa na mchezaji mwenza wa timu hiyo, Denis Kibu pamoja na Saido Ntibazonkiza wa Yanga.
Mbali na mbio hizo za ufungaji bora lakini, Mpole na wachezaji wenzake wanapambana vikali kuhakikisha Geita Gold inamaliza nafasi nne za juu ili kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, ambao Tanzania itaingiza timu nne.
Geita kwa sasa ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 35, moja nyuma ya Azam FC iliyopo juu yake kabla ya mechi za jana.