Inonga "Sikutaka Mayele 'Ateteme' "



BAADA ya kuonyesha kabumbu safi kwa kumkaba na kumnyima raha uwanjani mshambuliaji wa Yanga na kinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele, beki kisiki wa Simba, Henoc Inonga 'Varane' amesema hakuwa tayari kumuona Mcongoman mwenzake huyo, akitetema mbele yake katika pambano hilo la watani wa jadi '

Katika mchezo huo, ulioshuhudiwa miamba hiyo ikishindwa kufungana kwa mara ya pili msimu huu baada ya kutoka suluhu kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni kwa sasa.

Wiki moja kabla ya mchezo huo, Mayele aliahidi kuwa ana deni kwa mashabiki wake la kutimiza kuifunga Namungo FC na Simba, jambo ambalo alianza kulitimiza kwa kufunga dhidi ya timu hiyo ya Ruangwa mkoani Lindi na kusema sasa amebakiza kuitungua Simba, hivyo angeitungua juzi na kushangilia kwa staili yake ya kutetema.

Akizungumza na Nipashe baada ya mechi hiyo, Inonga alisema alilazimika kuhakikisha anakuwa makini na Mayele ili kutompa nafasi mshambuliaji huyo wa Yanga kutikisa nyavu zao halafu 'akatetema' mbele yake.

Inonga alisema amefanikiwa kumzuia na hakuweza kutetea na kwamba licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwa kila upande, lakini malengo yake ya kutompa nafasi mshambuliaji huyo kutimiza ahadi yake yalifanikiwa kwa asilimia 100.


"Tumepambana, malengo yalikuwa pointi tatu, lakini tumepata moja ila nimefanikiwa kumzuia mtu asiteteme (No kutetema), licha ya kutoka nchi moja na kuonyesha ni mechi ya upande wetu hakuweza kutetema," alisema Inonga.

Lakini wakati Inonga akiyasema hayo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alimtetea Mayele kwa kutofunga katika mchezo huo, akieleza ni jambo la kawaida licha ya kutoa ahadi kwa sababu malengo yao yalikuwa kutafuta pointi na hilo wamefanikiwa.

“Hii mechi ni kati ya Simba dhidi ya Yanga na si Mayele dhidi ya Inonga, hajafunga lakini tumepata pointi moja na kutufanya tuendelee kujiamini katika malengo yetu,” alisema Kaze.

Mayele ndiye kinara wa mabao hadi sasa kwenye Ligi Kuu msimu huu, akiwa amecheka na nyavu mara 12 akifuatiwa na George Mpole wa Geita Gold FC mwenye mabao 11.

Kwa matokeo ya mechi hiyo, yanaifanya Yanga kufikisha alama 55 kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakati huu ikibakiza mechi tisa kabla ya kufunga msimu huu, hata hivyo inafutiwa na Simba yenye pointi 42, lakini ikicheza mechi moja pungufu.

Simba itashuka tena dimbani kesho katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi kuwavaa wenyeji wao, Namungo FC waliopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi zao 29 zilizotokana na mechi 21.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad