WINGA wa Simba, raia wa Ghana, Bernard Morrison ‘BM3’ juzi mara baada ya Dabi ya Kariakoo alijikuta matatani kwa kushikiliwa kisha kuachiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumdhuru shabiki wa Yanga, hata hivyo jeshi hilo limesema shtaka lake bado linaendelea kuchunguzwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Tukio hilo limejiri usiku mara baada ya mchezo wao dhidi ya wenyeji Simba wakati nyota huyo akiwa njiani kurudi nyumbani, ikidaiwa chanzo ni shabiki huyo kumtania mchezaji huyo akimuita mwizi wa gari.
Baada ya Morrison kutaniwa hivyo, alishuka kwenye gari yake na kuanza kupambana na shabiki huyo kisha polisi kuwakatamata wawili hao kupelekwa kituo cha Polisi cha Chang’ombe kwa mashtaka.
Hata hivyo, mara baada ya kufikishwa kituoni hapo Mwanaspoti linafahamu Morrison alichukuliwa maelezo na kuachiwa kwa dhamana huku maofisa wa kituo hicho wakigoma kulizungumzia suala hilo
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ACP) Jumanne Muliro amelithibitishia Mwanaspoti jana, akisema Morrison na shabiki huyo bado wanaendelea kuchunguzwa wakiwa nje kwa dhamana baada ya tukio hilo.
“Hilo suala limetufikia kuna hayo malalamiko mimi nimeongea na wote wawili kwa maana ya Morrison na huyo shabiki, tumewahoji ingawa bado tunaendelea na uchunguzi zaidi na ukimalizika sheria zitachukuliwa,” alisema Muliro.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliisha kwa suluhu, huku Morrison akitolewa kipindi cha pili na kujikuta akizomewa na mashabiki wa Yanga, klabu aliyowahi kuichezea misimu miwili iliyopita