Ishu ya Morrison Kama Muvi, Akaliwa Vikao Vitatu



IMEISHA. Maisha ya soka ya Benard Morrison ndani ya Simba yamefikia mwisho ndani ya kikosi hicho baada kukitumikia kwa miaka miwili iliyoambatana na visa na mikasa mingi.

Simba jana ilitangaza kumpa Morrison mapumziko hadi mwisho wa msimu akamalize changamoto zake za kifamilia ambazo hawakuziweka wazi.

Ingawa utata kwenye taarifa ya klabu ulianzia kwenye maneno haya; “Simba inamtakia kila la heri Morrison katika mapumziko yake na safari yake ya soka hapo baadae.”

Morrison mwenyewe aliposti kwamba ana changamoto za kifamilia na akizimaliza atarejea kazini Msimbazi.


Morrison alisajiliwa Simba akitokea Yanga.

ISHU ILIVYOKUWA

Kocha Pablo Franco aliwaambia viongozi kwamba ; “Simtaki aondoke hata leo.” Mwanaspoti linafahamu kwamba juzi Alhamisi kulikuwa na vikao vitatu ndani ya klabu ya Simba. Asubuhi kilianza cha Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez dhidi ya Kocha Pablo Franco kilichofanyika kwenye ofisi za Simba Masaki.

Awali Mwanaspoti lilikujuza Pablo alipewa muda wa siku saba na uongozi wa Simba ili kukabidhi ripoti yake yenye mambo ya kiufundi kwa ajili ya msimu ujao yakiwemo kupendekeza wachezaji wapya na wa kuachwa.


Kwenye kikao hicho kilichofanyika kwa usiri mkubwa, Pablo alipendekeza Morrison kuwa mchezaji wa kwanza kuachwa na hilo utekelezaji wake ulianza Alhamisi kabla ya tamko la jana lililodai kwamba amepumzishwa.

Kikaoni mbali na kuweka wazi mipango yake, Pablo alitakiwa kusema mahitaji yake ya wachezaji wapya anaotaka wasajiliwe.

Mchana wa siku hiyo kulikuwa na kikao kingine cha pili kati ya Barbara na Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu.

Kikao cha tatu kilifanyika kambini baada ya mazoezi ya gym kumalizika Alhamisi jioni na kuhudhuriwa na benchi la ufundi pamoja na wachezaji wote.


Pablo ndio alikuwa akiongoza kikao hicho ambacho hakikuchukua zaidi ya dakika 15, aliwatangazia kuwa wachezaji kwamba Morrison hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kuanzia wakati huo ingawa hakuenda kiundani na hakuna aliyehoji.

Baada ya wachezaji kuelezwa jambo hilo walipewa ratiba ya mazoezi kila mmoja akisisitizwa kupambana na kujitolea kwenye mechi zilizokuwa mbele yao ili waweze kufanya vizuri kwani mkakati wao wa kupindua meza wanakimbizana nao kimyakimya.

Inaelezwa sababu za Simba kuachana na Morrison ni mwenendo mbaya na kiwango chake, kuchagua mechi za kucheza vizuri, utovu wa nidhamu na amekuwa na matukio mengi ya namna hiyo akidaiwa pia kutoroka kambini usiku.

Hata mawasiliano yake ya karibu na watu wa Yanga ni pamoja na mambo mengine.


Viongozi wa Simba wamekuwa wakikerwa na mambo hayo ikiwemo tukio lake la sasa la kutokuwepo kambini tangu alivyocheza mechi dhidi ya Yanga kwa kisingizio cha majeruhi wakati wengine wapo na wana programu maalum.

Simba watalazimika kumlipa stahiki zake zilizobaki zote hadi mwishoni mwa msimu. Morrison atakosa michezo saba ya kukamilisha msimu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad