Kapombe Achekelea Mechi 100, Bocco Akifunga Dakika 522



BEKI wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe, amesema limekuwa ni jambo la furaha kwake kutimiza mechi 100 alizocheza ndani ya klabu hiyo, tangu ajiunge tena akitokea Azam FC, akieleza tamu na chungu alizokutana nazo.

Kapombe ambaye alijiunga na Simba mwaka 2017, akitokea Azam FC, amesema halikuwa jambo rahisi kutoka Azam FC kutokana na mambo mengi waliyomfanyia, lakini mwisho wa siku maisha ni kama mzunguko, ilibidi arejee kwenye timu yake ya zamani ya Simba.

"Nashukuru kwangu ni jambo la furaha, si jambo dogo kufikisha mechi 100, namshukuru Mungu nimekuwa nacheza miaka yote kwa kiwango kikubwa, wapo waliocheza kwa miaka kama hii mitano sasa, lakini hawakufikisha michezo kama hii.
Nawashukuru walimu wangu wote waliopita, wachezaji na familia yangu, muhimu hapa ni kwamba nimetoa mchango mkubwa kwenye klabu na kutwaa mataji mbalimbali, ingawa ugumu niliokutana nao ilikuwa kuondoka Azam FC. Haikuwa rahisi kwa sababu walinifanyia vitu vingi vizuri," alisema.

Hata hivyo, mwaka 2017 haikuwa mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kuichezea Simba, kwani awali alijiunga na timu hiyo akitokea Polisi Morogoro na kuingia 2011, hadi 2013 alipokwenda nchini Ufaransa kwenye Klabu ya AS Cannes, alipodumu kwa mwaka mmoja, kabla ya kurejea na kujiunga na Azam mwaka 2014 hadi 2017, aliporejea kwenye klabu yake ya zamani, Simba.

Wakati huo huo, straika wa Simba, John Bocco amefunga bao lake la kwanza msimu huu kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.


Bocco alifungua akaunti yake kwenye mechi hiyo, akipachika bao la tatu dakika ya 82, kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting juzi usiku, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, timu yake ikishinda kwa mabao 4-1, akisubiri kufanya hivyo kwa dakika ya 522, siku 295 na michezo 13.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad