HALIMA Mdee na wenzake 18 wamesema wamefika kusikiliza rufaa zao wakisema “tuko tayari kwa lolote.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Rufaa hizo ni za kupinga kufukuzwa uanachama na kamati kuu ya Chadema kwa tuhuma za usaliti, kughushi na kujipeleka bungeni jijini Dodoma kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.
Mdee na wenzake wamefika katika ukumbi wa Mlimani City kunakofanyika kikao cha Baraza Kuu ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Kina Mdee wamefika ukumbini hapo saa saba kasoro wakiwa wamevalia kombati za kati ambazo ni vazi la Chadema wakiwa wanatembea kwa miguu.
Kulitokea vuta nikuvute mlangoni ambapo walikuwa na watu wakiwasindikiza waliozuiwa kuingia ndani.
Waliruhusiwa kuingiwa wao pekee na kwenda kukaa chumba maalum ambacho kimeandaliwa kwa ajili yao.
MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV limefika katika chumba hicho na kuzungumza na baadhi yao ambapo kila mmoja anasema,”tumekuja na tuko tayari kwa lolote.”
Nyakati zote, Mdee na wenzake wameonekana wenye nyuso za tabasamu.
Rufaa yao itasikilizwa ikiwa ni agenda ya sita ya kikao hicho cha Baraza Kuu kinachoendelea.
Mbali na Mdee aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.
Pia wamo, Hawa Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar na Katibu Mkuu, Bawacha-Bara, Jesca Kishoa
Wengine ni, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.
Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.