Wachezaji hao walikuwa sehemu ya kikosi kilichoanza katika michezo miwili iliyopita ya ligi dhidi ya Mbeya Kwanza na Biashara United wakiisaidia timu hiyo kuvuna pointi nne.
HATIMAYE Kocha Mkuu wa Yanga, Nasredine Nabi amefunguka kuhusu sakata la kuwatimua kambini mastaa wake Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo huku akijitetea kuwa alichukua uamuzi huo kwa manufaa ya timu kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Simba.
Saido na Ambundo waliondoshwa kwenye kambi ya timu hiyo iliyokuwa ikijiandaa na mchezo wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho dhidi ya Simba na kurejeshwa jijini Dar es Salaam.
Nabi amefunguka leo jijini Mwanza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa kesho ambapo amesema klabu kubwa inayojiheshimu lazima ifuate taratibu na misingi yake huku akiwatoa wasiwasi mashabiki kuwa kukosekana kwa nyota hao hakuwezi kuathiri kikosi chake.
Amesema licha ya kutimuliwa lakini nyota hao ni miongoni mwa wachezaji wenye nidhamu kikosini hivyo sakata hilo halimaanishi kuwa wamekuwa mzigo kwa klabu kwani wataendelea kuisaidia timu hiyo.
"Hakuna timu inayomtegemea mchezaji mmoja hata iwe mchangani, kwenye klabu kubwa na inayojiheshimu kuna utaratibu ambao kila mtu anaujua na kama haufuatwi ni tatizo kwahiyo huwezi kuacha kufuata utaratibu kwa sababu unatafuta matokeo". amesema Nabi na kuongeza.
"Ni kweli hicho kitu kimetokea lakini watu wanapaswa kujua wachezaji hawa hawakuwahi kuwa na tatizo hili la kinidhamu lakini kwa kuzingatia umuhimu wa mchezo na kuhitaji kudumisha utulivu kwenye timu tumelazimika kufanya hivyo, ni wachezaji wenye nidhamu siku zote wamekuwa na nidhamu na kuisaidia timu na wataendelea kuisaidia".
Nyota wa timu hiyo, Deus Kaseke amewatoa wasiwasi mashabiki wa Yanga kuwa kukosekana kwa wachezaji hao kutashusha morali ya Wana Jangwani huku akitamba kuwa Yanga ina kikosi kipana na kila mchezaji aliyesajiliwa amekidhi vigezo vya kuitetea klabu hiyo.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) utakaochezwa kesho saa 9:30 alasiri kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.