KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule ameondoka kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini hapa, akiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi akikwepa kupopolewa mawe na mashabiki wa timu hiyo, ambao walighadhabika baada ya timu hiyo kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union.
Tukio hilo limetoa baada ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC kumalizika ambapo baadhi ya mashabiki waliokuwa wameshika mawe walitaka kumpopoa wakimtuhumu kuwa na ugomvi na baadhi ya wachezaji.
Mashabiki hao walikuwa wanamtuhumu kutowatumia wachezaji muhimu ambao ni mshambuliaji, Paul Nonga na kiungo mshambuliaji, Peter Mapunda ambao ni miongoni mwa wachezaji ambao ana ugomvi nao.
Akizungumza na Nipashe Digital miongoni mwa mashabiki akiwamo, Mashaka Mwakajwanga amesema kufanya vibaya kwa kocha wa timu hiyo, kunahusishwa pia na kufanya mkataba wa kisirisiri na klabu nyingine ya nchi jirani ya Malawi kabla ya hata ya msimu kuisha.
Amesema kufanya vibaya kwa Mbeya City kunachagizwa na mambo mbalimbali ikiwamo uhasama baina ya wachezaji na kocha pamoja na kuhusishwa na kutia saini klabu nyingine.
“Tunahujumiwa na kocha wetu haiwezekani kwenye kikosi anashindwa kuwaweka wachezaji kama Paul Nonga na Peter Mapunda ambao kwa mchezo wa leo wangeipatia matokeo mazuri timu yetu, bifu lake na wachezaji linaigharimu klabu yetu ambayo kwenye mzunguko wa kwanza ilifanya vizuri,” amesema Mwakajwanga.
Baraka Mwangisi amesema kwa matokeo ya Mbeya city kukubali vichapo mara tatu mfululizo kunaiweka kwenye hali mbaya katika msimamo wa ligi kuu ya NBC.
Amesema kwa mwenendo huo Kocha Lule anapaswa kujitathmini kama anafaa kuendelea kukinoa kikosi hicho au kuondoka kutokana na matokeo mabaya ambayo yanawaumiza mashabiki na kuhisi ni hujuma zinafanyiwa.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Timu ya Mbeya city, Lule amesema jukumu lake ni kuitengeneza timu kiufundi na sio kusikiliza maneno ya mashabiki huku akisisitiza kuwa timu yake ilitengeneza nafasi nyingi lakini ikashindwa kuzitumia.
Ameongeza pamoja na matokeo kutokuwa mazuri lakini bado timu hiyo ina nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kubakiwa na michezo minne ambayo miwili itachezwa nyumbani na miwili ugenini.
“Kazi tunayoifanya sasa hivi ni kuitengeneza timu, tumetengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia lakini wenzetu wametengeneza nafasi moja na wakaitumia vizuri, tutaendelea kurekebisha makosa katika michezo iliyobaki ili tupate mafanikio,” ameongeza Lule.
Kwa upande wake Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema pamoja na kupata ushindi lakini walipata wakati mgumu kutokana na kucheza mchezo huo mchana wakati wa jua kali.
Hata hivyo amedai matokeo waliyoyapata kwenye mchezo huo ni kipimo kizuri cha timu yake kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya wanalambalamba Azam FC.
Amewapongeza wachezaji wa timu yake kwa kucheza vizuri na kupata matokeo ambayo yamewaweka katika nafasi nzuri.