Kocha wa Simba Pablo Afunguka Tetesi Kutua Orlando Pirates



HUKU tetesi zikizidi kuvuma kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amepata ofa ya kwenda kuinoa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Nipashe limebisha hodi kwa kocha huyo kutaka kujua ukweli kuhusu suala hilo na msimamo wake.

Orlando Pirates kwa sasa ipo chini ya kocha wa muda, Mandla Ncikazi, ambaye anaonekana kukalia kuti kavu kutokana na mashabiki wa timu hiyo kutomkubali, sababu ikiwa ni mwenendo mbaya kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini, wakati huu ikiwa nafasi ya sita na alama zake 40 baada ya mechi 27.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, Pablo alipata kigugumizi kujibu kutakiwa na Orlando Pirates na timu nyingine zinazodaiwa kuhitaji huduma yake.

"Hizo ni tetesi kwa sasa siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu mimi ni muajiriwa wa klabu ya Simba," alisema kwa kifupi kocha huyo raia wa Hispania.

Kuhusu mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Pablo aliweka wazi kuwa bado hawajakata tamaa kwa sababu wana mechi nane zilizobaki kabla ya msimu kumalizika.


Pablo alisema ingawa wapo nyuma kwa alama 10 dhidi ya vinara Yanga, lakini kwa kuwa bado wana idadi kubwa ya michezo iliyobaki lolote linaweza kutokea.

Alisema baada ya kutoka sare dhidi ya Yanga katika mchezo uliopita walijiweka katika mazingira magumu ya kutete ubingwa kutokana na ratiba kubana, lakini hata kwa wanaongoza lolote linaweza kutokea.

"Kama nilivyowahi kusema huko nyuma mbio za ubingwa bado zipo wazi, tupo nyuma kwa pointi 10, lakini kama wanaongoza wataendelea kudondosha pointi na sisi tukishinda zetu, tunaweza kutetea ubingwa.


"Nimefurahi kwa ushindi huu mnono, mchezo ulikuwa mzuri tumetengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza, lakini hatukuzitumia vizuri, tulivyorudi cha pili tulirekebishs makosa na kufanikishs ushindi huu," alisema Pablo huku akifunguka kuwa amefurahi kuona mshambuliaji wake, John Bocco amepata bao lake la kwanza jambo ambalo limerejesha morali ndani ya timu hiyo na mchezaji husika.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa, alisema ulikuwa mchezo mzuri, lakini wamepoteza kutokana na uzoefu wa kikosi cha Simba, lakini wanajipanga kwa ajili ya michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Bara.

“Tulikuwa vizuri kipindi cha kwanza kama tungeendelea na ubora ule tungefanya kitu, kipindi cha pili wachezaji walikuwa wamechoka wakawa wanashindwa kukaba, bado tuna nafasi ya kushinda katika michezo iliyosalia hatuwezi kushindana na Simba ni timu kubwa iliyokaa pamoja muda mrefu.

“Simba wametushinda kutokana na uzoefu wao, sisi tuna timu changa ambayo inajipanga, pointi moja ya Yanga tuliyopata Kigoma imetuponza tumetembea kilomita 2800, hivyo tulikuwa na uchovu japokuwa siwezi kusema hii ndiyo iliyotugharimu,” alisema Mkwasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad