Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi aliyesimamishwa, James Mbatia
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi aliyesimamishwa, James Mbatia amemjibu mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Joseph Selasini ambaye siku za hivi karibuni alimtuhumu mambo mbalimbali, ikiwamo kuwa na uhusiano na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mei 26, wakati akizungumza na waandishi wa habari, Selasini alisema halmashauri kuu ya chama hicho, iliazimia na kumtaka Mbatia kuacha uhusiano wake na CCM.
Alisema yeye na Antony Komu baada ya kutoka Chadema na kujiunga na NCCR Mageuzi, Juni 2020, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu Mbatia aliwapeleka nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally eneo la Kilimani jijini Dodoma.
Apangua madai
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam jana, Mbatia aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchunguza madai yaliyotolewa na mjumbe huyo na kuchukua hatua za kisheria.
Alisema Ofisi ya Rais ni taasisi na sio ofisi binafsi na kuviomba vyombo vinavyohusika, kufanya uchunguzi wa kina na kutoka hadharani kuthibitisha madai hayo.
“Leo mtu anatoka hadharani na kusema mara nimepewa Sh800 milioni, mara Sh500 milioni. Rai yangu kwa Takukuru na Ofisi ya Rais, wafanye uchunguzi wa kina na ikithibitika walete mashtaka dhidi yangu,” alisema Mbatia.
Kuhusu madai ya kuomba kuteuliwa kuwa mbunge, Mbatia alizitaka mamlaka zinazohusika pia kufanya uchunguzi wa kina ni namna gani alivyoomba uteuzi huo.
“Sikuwahi kuwasiliana na hayati John Magufuli, zaidi ya Julai 22, 2020 wakati akifungua jengo la uchaguzi na mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD).
“Rais ni taasisi, unapomtaja Rais unafanya asiaminike, na mambo yote haya yalifanywa na maofisa wa Serikali, mara chama kiliahidiwa majimbo 20 yako wapi? Tupewe 800 milioni na majimbo kweli?” alihoji.
Mbatia alisema hadi leo hajapewa tuhuma zinazomkabili kwa maandishi, licha ya kusikia amesimamishwa nafasi ya uwenyekiti na kikao kilichojita cha halmashauri kuu.
“Niiombe Idara ya Usalama wa Taifa, Takukuru na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi nyumbani kwangu na kuonyesha chumba ambacho kinadaiwa kipo kwa ajili ya kuwatesa watu, kama inavyodaiwa nilimtesa Katibu Mkuu wangu.
“Vyombo vinavyohusika na jinai vije nyumbani kwangu, kwa ajili ya kuthibitisha hicho chumba, maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kuvuruga amani ya nchi yetu, nilikuwa nisijibu, lakini leo tuhuma hizi zimetolewa mbele ya vyombo vya habari na maofisa wa Serikali wakiwepo,” alisema.
Komu naye afunguka
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Bara, Anthony Komu alisema tuhuma zinazoelekezwa kwake kuwa sio mwanachama wa NCCR sio kweli, kwani kadi namba saba alipewa na Elizabeth Mhagama baada ya kutimiza vigezo vyote.
Alibainisha kuwa baada ya kupewa kadi hiyo aligombea ubunge ambao ulithibitishwa na maofisa wa serikali kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Ofisa wa Serikali alifanya mambo yake, leo anasimama mtu anasema mimi sio mwanachama wa NCCR-Mageuzi, nilipitishwaje kugombea ubunge kama mimi sio mwanachama?” alihoji Komu ambaye naye alisema amesimamishwa pasipo kujulishwa kwa barua yoyote.
Kuhusu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutumika alisema, baadhi ya watendaji walioko chini yake wamekuwa wakitumika kwa maslahi binafsi.
Alibainisha kuwa kikao kinachojihalalishia mambo ni cha halmashauri kuu ya NCCR, lakini hakiwezi kukutana kwa dakika 40, halafu kikajadili ajenda pamoja na maazimio tena kukiwa na kiongozi wa Serikali.
“Kwa hili kama chama tumeazimia kumwandikia Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene pamoja na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD) kumueleza hili,” alisema Komu.
Naye mjumbe wa bodi ya wadhamini, Sam Ruhuza akizungumzia madai ya kuuzwa kwa mali za chama alisema, baraza ndilo lenye mamlaka ya mali za chama ndio maana likasajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema kama chama hicho kingegundua kuna jinai yoyote, kingekuwa kimeshachukua hatua.
“Ajenda ya mali za chama ingeletwa kwenye chama, kwa nini ipelekwe kwa waandishi wa habari? Mimi ni kinara wa demokrasia hapa nchini, utaratibu ni kwamba sekretarieti inaandaa ajenda kwenda kamati kuu, nayo kamati kuu inaandaa kwenda halmashauri kuu, na mimi kama mjumbe sikuwahi kupewa taarifa ya kikao,” alisema Ruhuza.
Mwanzo wa mgogoro
Mei 21 mwaka huu halmashauri kuu ya chama hicho iliyokutana katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu Kurasini jijini Dar es Salaam iliazimia kumsimamisha Mbatia na Makamu Mwenyekiti wake (Bara) kujihusisha na shughuli za chama.
Hata hivyo, Mei 22 kamati kuu ya halmashauri kuu ya chama hicho, ilikutana na kutoa maazimio manne, ikiwamo kuwasimamisha uongozi Makamu mwenyekiti (Zanzibar) Ambar Hamid, mweka hazina Suzan Masele na naibu Katibu mkuu (Zanzibar) Amer Mshindan.
Mei 25, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, iliridhia kusimamishwa kwa Mbatia na sekretarieti yake yote, hadi uamuzi utakapoamuliwa.