Kumekucha..Nabi Atoa Kigezo Kizito cha Usajili Mpya Yanga



YANGA inalikaribia taji la 28 la Ligi Kuu Bara ikibakiza hatua chache tu na kocha wake, Nasreddine Nabi ametoa masharti mapya ya usajili wake.

Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema timu yake itahitaji watu wachache wapya kuongeza nguvu haswa kimataifa lakini usajili huo hautampa nafasi staa yeyote ambaye alikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu bila kucheza. Awe wa kigeni au mzawa.

Nabi alisema hawatarudia makosa ya kuchukua mchezaji ambaye hata kama ni bora lakini hakuwa anacheza soka la ushindani kwani muda wa kujiandaa na msimu ujao kwa ndani na kimataifa ni mfupi.

“Ukiangalia ligi hapa itaisha mwezi Juni, tutahitaji muda pia wachezaji kupumzika lakini mapumziko hayo hayatakuwa marefu kutokana na kalenda ya msimu ujao hasa mashindano ya Afrika iko karibu sana,” alisema Nabi ambaye timu yake itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza kati ya Septemba na Oktoba.


“Hali hii sio afya kumchukua mchezaji ambaye alikuwa hachezi soka la ushindani huko anakotoka, tunahitaji kuingiza mtu bora ambaye alikuwa anapata nafasi ya kucheza ili aje kuendelea hapa.

“Kuna uamuzi tuliufanya hapo nyuma umetupa kitu cha kujifunza, mashabiki wetu hawatatuelewa kama tukiendelea kufanya makosa ya namna hiyo, hii ni timu inayoongozwa na viongozi,wanachama na mashabiki wenye kiu kubwa ya mafanikio,” alisema Nabi.

Yanga ilimsajili winga Chico Ushindi kutoka TP Mazembe ambaye licha ya kuwa na kipaji kikubwa lakini kukosa kwake kucheza ndani ya timu hiyo ya DR Congo alishindwa kufanya kazi bora ndani ya Yanga.


Masharti hayo ya Nabi yanamuweka beki wa kushoto wa Uganda, Mustapha Kiiza katika nafasi ngumu ya kusajiliwa na timu hiyo licha ya kuwa chaguo lao kwani amekuwa nje ya uwanja kwa muda wa zaidi ya miezi sita.

Mwanaspoti linafahamu kwamba tangu Kiiza asajiliwe na CF Montreal ya Ligi Kuu ya Marekani hakuwa anacheza kwa muda mrefu hatua ambayo kulingana na masharti hayo ya Nabi yanamuondoa beki huyo kulamba dili hilo.

Mapema Kiiza kabla ya kutua CF Montreal akitokea KCCA, Yanga kupitia injinia Hersi Said iliwahi kumuhitaji lakini beki huyo akawapiga kona kisha kuelekea Marekani.

Yanga inasaka beki wa kushoto wa maana ambaye ataondoa changamoto za nafasi hiyo baada ya kuyumba kwa mabeki wao Yassin Mustapha na David Brayson huku winga wa kushoto Farid Mussa akipewa eneo hilo mara kadhaa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad