MZEE Yohana Tano Nabii mwenye umri wa miaka 82, kutoka kijiji cha Nandolia kaunti ya Bungoma nchini Kenya amekuwa gumzo ndani na nje ya nchi hiyo baada ya kudai kuwa anawaponya watu wanaougua UKIMWI, saratani, ukoma na majeraha. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).
Mzee huyo ambaye anajiita Nabii mbali na kudai kuwa anatibu magonjwa hayo, pia amewaacha wengi vinywa wazi kutokana na uwingi wa wake zake ambao sasa wamefikia 42 huku akiwa na watoto 289.
Catherine Nalonja mke wa 10 wa Yohana Nabii
Cha kushangaza Nabii huyo ambaye jina lake halisi ni Ronald Nakalila Wanyama, amesema bado ana mpango wa kuongeza wake wengine ilihali mke wake wa mwisho sasa ambaye ni binti mbichi wa miaka 24 akiwa na ujauzito wa miezi sita.
Katika mahojiano yake na gazeti la Star la nchini humo, Nabii huyo ameeleza jinsi alivyowaponya wateja wake wengi kwa kutumia dawa za mitishamba.
Amesema anahudumia angalau watu 70,000 kwa mwaka. Nabii huyo ambaye pia ana kanisa lake linalofahamika kwa jina la Muungano, amesema amekuwa akiwaunganisha wanaume na wanawake ambao wametalikiana.
Nabii amesema ana Biblia yake, ambayo ina vitabu 69 ambavyo anatumia kufundisha waumini wake katika Kanisa la Muungano.
“Huduma zangu zote zinahusiana na Biblia. Mimi ndiye mtu pekee wa Mungu ambaye nitabadilisha injili ya ulimwengu huu,” amesema.
Bendera ya kanisa la Muungano
Nabii amesema alizaliwa mwaka 1940 katika eneo ambalo sasa ni eneo bunge la Saboti katika kaunti ya Trans- Nzoia. Babake baadaye alihamia Kanduyi katika kaunti ya Bungoma alipokuwa na umri wa miaka minane kabla ya (Nabii) kuachana na familia yake ili kumtumikia Mungu.
“Kumtumikia Bwana ni jambo ambalo nilianza muda mrefu uliopita na sijawahi kukata tamaa,” amesema na kuongeza kwamba amekuwa katika utumishi kwa miaka 62.
Nabii ameongeza kuwa Mungu alimpa uwezo wa kutabiri, kuombea wagonjwa na kutibu wagonjwa kwa dawa za mitishamba.
Amesema amewaombea mamilioni ya watu kutoka pande zote za dunia. Nabii pia huwa anahudumia wateja bila malipo bila kuomba pesa taslimu, akisema kuwa ni zawadi aliyopewa na Mungu na hataruhusu wateja kumlipa.
Nabii ana nyumba tano: tatu Bungoma (Nandolia, Matulo na Webuye), Kitale na Lugari kaunti ya Kakamega.
Nabii ana kanisa lake katika nyumba yake lenye wodi za kulaza wagonjwa walio katika hali mbaya.
“Dawa hizi wakati mwingine zina madhara kwa mwili kwa hiyo katika nyumba yangu nimetenga baadhi ya vyumba ambavyo wagonjwa wanaweza kupumzika na kufanyiwa maombi,” amesema.
Baada ya kuwaombea wagonjwa, anahamia Mto Chwele na kuwabatiza kwa maji, akisema ni njia ya kuosha dhambi zao. “Ninalo shamba kubwa na rasilimali za kutosha kufadhili familia yangu,” amesema.
Mke wa 10 wa Nabii, Catherine Nalonja, ambaye ni mama wa watoto watano, amesema aliolewa mwaka wa 2002.
Wake wote 42 wanakaa na wana uhusiano mzuri na nabii. Ameongeza kuwa Nabii hana tatizo la kuhudumia familia.