Mshambuliaji wa klabu ya PSG Kylian Mbappe amesema kuwa kitendo cha yeye kuamua kubaki kwenye timu hiyo hakijachagizwa na pesa bali ni mazungumzo ya maendeleo ambayo klabu hiyo inataka kufanya.
Mbappe ameweka wazi kilichomfanya akubali kusalia kwenye klabu ya Paris Saint-Germain licha ya kufanya makubaliano ya mdomo na Rais wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez.
“Tumezungumza kwa mwezi sasa na mkuregenzi wa michezo kuhusu miradi ya maendeleo ya soka na tumetumia muda mchache sana kuzungumzia pesa. Mimi natokea nchi ya Ufaransa, sehemu ambayo nataka kuishi, kuzeekea na kuamalizia maisha yangu ya soka. Kuondoka haikuwa sawa ni rahisi kuweza kupumbazika kwenye hili, hii ni nchi yangu.
“Mradi wa soka unakwenda kubadilika, klabu inataka mabadiliko na naamini hadithi yangu bado haijaisha , kuna kurasa nahitaji kuziandika bado.” - amesema Mbappe akizungumza na mmoja ya waandishi wakongwe Ulaya Guillem Balague.
Aidha, pia Mbappe amesema licha ya kuwa amechagua kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kukitumikia kikosi cha Paris St-Germain lakini bado ana mpango wa siku moja kwenda kucheza Real Madrid.
“Hauwezi kujua lipi litatokea baadaye”, alisema Mbappe mchezaji wa zamani wa Monaco na kuongeza, “Sifikirii ya mbele, nafikiria ya sasa ambayo ni kwamba nimeongeza mkataba mpya wa miaka mitatu hapa Paris St-Germain”.