Ule mzizi wa fitina kwa watani wa jadi Simba na Yanga utakatwa leo, zitakapocheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Timu hizo zimetoka sare kwenye mechi zote mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, hivyo ya leo itaamua nani mbabe msimu huu, kwani ni lazima mshindi apatikane.
Kama zitatoka sare ya aina yoyote, zitalazimika kupigiana penalti tano tano ili kumpata mshindi atakayetinga hatua ya fainali, ikizisubiri Azam FC na Coastal Union zitakazocheza kesho, kabla ya mechi ya fainali itakayochezwa Julai 2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana kwenye mechi ya nusu fainali ya kombe hilo ni Julai 12, 2020 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikiichapa Yanga mabao 4-1.
Msimu uliopita, timu hizo zilikutana tena kwenye kombe hilo, lakini safari hi ilikuwa ni fainali kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Julai 25 mwaka jana, Simba ikishinda tena bao 1-0.
Je nani kwenda fainali leo⁉️ Nini ubashiri wako