Mwanza. Imeelezwa kuwa wafanyakazi 39 kati ya 813 waliokuwa wameajiriwa katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM Kigogo Busisi wameukimbia mradi huo na kuajiriwa kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza Isaka.
Hayo yemeelezwa leo Mei 7 na mkandarasi mshauri wa mradi huo, Benjamin Michael mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo.
Mradi huo unaojengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya zaidi ya Sh716 bilioni umefikia asilimia 43.
Takwimu hiyo inafanya wafanyakazi waliosalia kwenye mradi huo kuwa ni 774, jambo linalopunguza ufanisi katika utekelezaji wa mradi huo.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema mkoani humo, Hamisi Tabasamu amesema katika mradi huo kuna changamoto lukuki ikiwemo ujira mdogo na mkandarasi kutotoa mikataba kwa wafanyakazi wake.
Kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani humo, Boniphace Mkumbo na wawakilishi wa kampuni ya CCECC pamoja na mkandarasi mshauri wa mradi huo kuwalipa wafanyakazi hao.
"Wananchi msisite kusema na kupongeza mnapoona mambo yanaenda vizuri, dhamira ya serikali ni kuona ilani ya CCM inatekelezwa kama ilivyoelekezwa. Japo mwenendo wa mradi huu siyo mbaya ila tunahitaji kuona watanzania walioajiriwa kwenye miradi hii wanapata manufaa kutokaana na miradi hiyo," amesema Majaliwa.
Ametahadharisha kwamba hategemei kusikia changamoto hizo zikijirudia atakaporudi kukagua mradi huo huku akikemea tabia za wizi wa vifaa vya ujenzi unaifanywa na baadhi ya watu waliopo katika mradi huo.
"Msiruhusu nikirudi nikute wafanyakazi wanaondoka hapa.
Patawaka moto mtatafuta mbebeo wa kuwabeba hapa. Wafanyakazi wanapungua tunataka wafanyakazi waongezeke ili mradi ukamilike kwa wakati," amesema Majaliwa