Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali itashirikiana na mgunduzi wa gari inayotumia umeme Ali Masoud ‘Masoud Kipanya’ ili kuiwezesha bidhaa yake hiyo kuingia sokoni.
Profesa Mkenda ameyasema hayo katika mdahalo wa wiki ya ubunifu inayoenda sambamba na Mashindano ya Ubunifu, Sayansi na Teknolojia (Makisatu).
Mdahalo huo umeandaliwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jijini Dodoma.
“Masoud amechukua miaka 10 kufanya ubunifu wake tunaouona, sasa hivi tutashikana naye mkono kuhakikisha kuwa anaweza kutengeneza kama bidhaa na ikaanza kuingia sokoni,”amesema.
Amesema Masoud amewaeleza kuwa anataka mashine inayoweza kutengeneza cover za magari ambayo inauzwa kwa gharama kubwa.
Amesema kutokana na hitaji hilo, Serikali inaangalia uwezekano wa Taasisi ya Teknolojia ambayo nayo itakuwa na kampuni tanzu iweze kununua mashine kwa ajili ya kutengeza cover za magari.
Waziri huyo amesema wanaangalia uwezekano huo wa kuinunua mashine hiyo kwasababu itatumiwa pia na wabunifu wengine ambao watataka kutengeneza cover za magari, pikipiki na kadhalika.
Profesa Mkenda alisema kwa kufanya hivyo kutamwezesha Masoud kutumia mashine hiyo katika kuendelea ubunifu wake na Taifa likasonga mbele.
Amesema mbunifu huo na wengine wanaohitaji fedha Serikalini watasaidiwa ili waweze kuingiza bidhaa zao sokoni.
Amesema wataangalia pia ufadhili wa benki ama mtu yoyote atakayeweza kumsaidia mbunifu huyo ili asonge mbele.
“Sio suala la fedha za umma bali ubunifu ukishakuwa mzuri unaokubalika na watu unauzika,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa COSTECH, Dk Amos Nungu amesema wiki ya Ubunifu ni sehemu muhimu kwa kuendelea kuchagiza Ubunifu wenye tija katika maendeleo ya nchi.
Amesema wiki hiyo inatoa nafasi kubwa Kwa wabunifu kuendelea kujuana baina katika kupanua bunifu wanazozifanya.
Katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali imetenga Sh5.5 bilioni kwa ajili ya kuendeleza ubunifu nchini.