UONGOZI wa Mbeya Kwanza umesema mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya vinara Yanga, utakuwa mgumu huku wakimkosa mchezaji wao muhimu, Enock Jiah ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyopita.
Yanga.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Mbeya Kwanza, Mohamed Mashango, alisema mchezo utakuwa na ushindani kwa sababu wao ni wageni na wanashiriki mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Mchezo utakuwa mgumu, tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ambayo haijafungwa mpaka sasa, vilevile ina kikosi kipana hivyo lazima tuingie kwa tahadhari," alisema Mashango.
Mwenyekiti huyo alisema kikosi chake kinaendelea na mazoezi ya mwisho kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo na anaamini wachezaji wakifuata vyema maelekezo ya benchi ya ufundi watapata matokeo mazuri.
Alisema baada ya aliyekuwa Kocha wao mkuu, Mbwana Makata kufungiwa kutojihusisha na mpira kwa muda wa miaka mitano, uamuzi huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa wachezaji pamoja na benchi zima la ufundi.
"Taarifa hiyo imetuathiri sisi pamoja na benchi zima la ufundi, baada ya michezo yetu miwili tutafanya mpango wa kumtafuta mbadala wa Makata isipokuwa kwa sasa timu ipo chini ya kocha wetu msaidizi," Mashango alisema.
Makata alipata adhabu hiyo baada ya kubainika kuwashawishi wachezaji kugomea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo iliyopangwa kuchezwa Ijumaa iliyopita kwa madai hakuna gari la wagonjwa.
Kiongozi mwingine wa timu hiyo aliyekumbana na adhabu ya kifungo ni meneja, David Naftali.
Tayari Namungo FC imepewa pointi tatu na mabao matatu kufuatia wageni Mbeya Kwanza kugomea mchezo huo uliotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Mbeya.