MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, leo inatarajia kutoa hukumu ya rufani namba 129, katika kesi ya jinai iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wa wawili.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Silvester Nyegu na Daniel Mbura, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi kwa kutumia silaha.
Februari 14, mwaka huu, mahakama hiyo ilianza kusikiliza hoja 14 za waleta rufani kupinga adhabu ya hukumu ya kifungo cha miaka 30 kwenda jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Arusha.
Oktoba 15, mwaka 2021, Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Odira Amworo, alimtia hatiani Ole Sabaya na wenzake kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Katika rufani hiyo, mawakili wa wapeleka rufani katika kesi hiyo, walikuwa ni Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Majura Magafu, Edmund Ngemela, Silvester Kahunduka na Fridolin Bwemelo.
Kadhalika, katika kesi hiyo, mawakili wa wajibu rufani ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmedy Mtenga, Wakili wa Serikali, Baraka Mgaya na Wakili wa Serikali, Veridia Mlenza, na rufani ilisikilizwa chini ya Jaji wa mahakama hiyo, Sedekia Kisanya, kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma.
Wakati akitoa hukumu hiyo, hakimu Amworo, alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani huko, mahakama imewatia hatiani na kuwahukumu miaka 30 kwenda jela kwa kutenda makosa matatu.
Alisema kosa la kwanza na la pili ni la unyang’anyi wa makundi pasipo kutumia silaha, na kosa hilo lilifanywa na washtakiwa wote kwa pamoja kwa kuwa waliwatendea Numan Yasin na Ramadhani Rashid (mashahidi wa Jamhuri), katika duka la Mohamed Saad, lililoko Mtaa wa Bondeni, jijini Arusha.
Kosa la tatu alisema ni la unyang’anyi wa kutumia silaha ambalo washtakiwa hao, walimtendea Bakari Msangi, kwa kumpiga, kumfunga pingu, kumtishia silaha na kumpora fedha Sh. 390,000.
Hakimu alisema hakuna ubishi kwamba Sabaya akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, alitenda makosa hayo kinyume na sheria.
Pia, alisema kwa kuwa mikono yake imefungwa na sheria hawezi kutoa adhabu ya zaidi ya kifungo cha miaka 30 japokuwa wametiwa hatiani kwa makosa matatu ambayo kila kosa kifungo chake ni miaka 30 na watatumikia adhabu hiyo kwa pamoja.
Alisema kosa la kwanza, la pili na la tatu ni kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa na wakati mwingine kifungo kinakwenda sambamba na adhabu ya viboko hivyo alikataa ombi la wakili wa Jamhuri kifungo kwenda sambamba na viboko.
Sabaya na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kwanza la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Ilidaiwa mahakamani huko Februali 9, mwaka 2021, wakiwa Mtaa wa Bondeni, Jiji la Arusha, katika duka la Sahiid Store, wote kwa pamoja wakiwa na silaha walifanikiwa kumpora Bakari Msangi, Sh. 390,000 na simu mbili na kabla ya uporaji walimshambulia kwa kumpiga ngumi, mateke, kofi na kumtishia kwa silaha.
Shtaka la pili lilikuwa linawakabili wote kwa pamoja na ilidaiwa kwamba Februali 9, mwaka 2021, walipora fedha kaunta katika duka la Mohamed Al Saad, Sh. 2,769,000 na kabla ya uporaji waliwapiga mateke, makofi na kuwatisha kwa silaha watu waliokuwapo na kuchukua kiasi hicho cha fedha.
Shtaka la tatu unyang’anyi wa kutumia silaha lilikuwa likiwakabili washtakiwa wote.
Ilidaiwa mahakamani huko, Februari 9, mwaka 2021, katika Mtaa wa Bondeni, jijini Arusha wakiwa na silaha walipora simu moja ya mkononi, Sh. 35,000 mali ya Ramadhani Rashid na kabla ya kufanya uhalifu huo waliwaweka chini ya ulinzi watu wote waliokuwa ndani ya duka la Mohamed Saad.