Mbunge Mpina Acharuka Bungeni



By Sharon Sauwa
Dodoma. Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amewataka wabunge kukataa kulipa Sh356 bilioni kwa Kampuni ya Kuzaliza Umeme ya Symbion hadi hapo ukaguzi na uchunguzi utakapofanyika kuhusu kilichojificha katika swala hilo.

Mpina ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ameyasema hayo leo Jumatatu wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema kuwa Serikali inatakiwa kulipa Sh356 bilioni kwa kampuni ya kuzalisha umeme ya Symbion wakati hawajaambiwa waliohusika katika kuingia katika mkataba huo mbovu wamechukuliwa hatua gani.

“Anapigiwa chapuo bila kuambiwa malimbikizo yake ya kodi ni shilingi ngapi. Inapigwa chapuo hatuambiwi ni ukaguzi gani uliojificha nyuma ya pazia hili,”amesema.


Amewataka wabunge kukataa mikataba na malipo hayo hadi hapo uchunguzi na ukaguzi utakapofanyika juu ya kilichojificha kwenye suala hilo.

“Tujue mazagazaga yote yaliyojificha katika jambo hilo na haki zetu zilizopo katika jambo hilo. Lakini mikataba yote mibovu iitishwe tuweze kuifuta,”amesema.

Kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa nchini, Mpina amesema matatizo mengine yaliyosababisha bei za bidhaa kupanda nchini yametengenezwa na watendaji wasio waadilifu.


“Kama kuna upandaji holela wa bei na waziri anajua na tuna FCC (Tume ya Ushindani wa Bishara), hawa watu wanaopandisha bei kiholela kwanini hawajachukuliwa hatua?”alihoji.

Amesema Waziri (bila kumtaja) anawafahamu waagizaji wa mafuta nje ya nchi na wazalishaji wa ngano ndani na nje ya nchi na kuhoji hao waliopandisha bei holela kwanini hawajachukuliwa hatua.

“Waziri kwanini anawaogopa hawa? Au anataka kutuambia kuwa hawa watu wana nguvu kuliko Serikali? Au waziri anaubia nao na kuwaacha watanzania na kuteseka na mfumko mkubwa wa bei,”alisema.

Amesema mara 10 ndani ya saa nne uzalisjhaji unashuka na watapandisha bei ili kufidia hasara.


Pia amesema kulikuwa na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu kuwa kuna wizi wa mafuta mkubwa kwenye Wakala wa Ununuzi wa Pamoja wa Mafuta na kwamba alitegemea kuwa ukaguzi wa haraka ungefanyika ili kujua ukweli.

Hata hivyo, amesema hoja inatolewa kwenye wezi inapelekwa katika tozo zilizoko katika mafuta ambazo zinasaidia katika miradi ya maendeleo nchini.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad