Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa amemwaga machozi bungeni wakati akieleza kuwa Kampuni ya Syno Hydro iliyopopewa zabuni ya kujenga barabara ya mwendokasi kuanzia Kariakoo hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam imevurunda katika miradi mingine.
Silaa amesema hayo leo Jumatatu Mei 23, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mwaka 2022/2023.
Amesema kuwa kampuni hiyo imepewa miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo maji lakini imekuwa akichelewesha kukamilisha kazi na kuchelewesha malipo ya wafanyakazi wao.
Amesema katika barabara imegundulika kuwa umbali wa kilometa 2.5 katika barabara ya mwendo kasi ya Gerezani hadi Mbagala walibaini ubovu wa barabara hiyo.
Hata hivyo wabunge walilisemea jambo hilo na kuieleza Serikali na hivyo kurekebishwa.
Amesema licha ya dosari hizo mkandarasi huyo amepewa zabuni ya kujenga barabara ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Gongo la Mboto.
“Kama viongozi wasingesimama na kusema hapa pabovu mkandarasi angeendelea huko wakati mwingine Serikali tuwe tunaangalia mkandarasi anakazi zaidi ya moja na kwenye maeneo mengi wanavuruga,”amesema.
Amesema mkandarasi huyo amepewa kazi nyingine ya kujenga barabara ya mwendo kasi ya kilometa 23.6 ya kutoka Kariakoo hadi Gongo la Mboto.
“Bunge lako hili linaenda kutekeleza kero ambayo iko Mbagala iko Temeke litakuwa Bunge la namna gani? Mkuu wa Wilaya ya Temeke alikwenda kusimamia walipwe wafanyakazi, Tanroad (Wakala wa Barabara Nchini) wakamuandikia barua asiingilie mkataba huo,”amesema.
Amehoji kama mkataba waliosaini kati yao na Tanroads unasema mkandarasi asilipe haki ya wafanyakazi.
“Halafu ukisema unaonekana kuwa unajambo lako binafsi. Hatuwezi kukubaliana na hilo,”amesema.
Amesema wao hawapingani na utaratibu wa utoaji wa zabuni ili wanachopinga ni uadilifu wa watendaji wanaosimamia zabuni hizo.
“Sisi tunaenda kwenda kwenye uchaguzi,”amemalizia Silaa na kuanza kulia na kisha kukaa kwenye kiti huku akiwa amefunika macho yake.