Mshambuliaji wa kutoka nchini Burundi Amis Tambwe metuma salamu kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuiwezesha DTB FC kupanda Daraja, ikitokea Ligi Daraja la Kwanza msimu huu 2021/22.
DTB FC jana Jumapili (Mei 08) ilijihakikishia kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2022/23, baada ya kuichapa Pamba FC ya jijini Mwanza bao 1-0, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.
Tambwe ambaye aliwahi kuzitumikia Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti amesema wanakwenda Ligi Kuu msimu ujao wakiwa na matumaini ya kupambana ili kujiweka katika nafasi nzuri na kuifanya timu yao kuwa bora miongoni mwa timu bora za Daraja hilo.
Amesema ni vigumu kwa DTB kwa sasa kusema wanakwenda kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu, kutokana na ugeni ambao watakua nao katika ligi hiyo, lakini dhumuni lao kubwa litakua ni kuhakikisha timu yao inamaliza kwenye nafasi nzuri.
“Haiwezekani tukasema tunakwenda Ligi Kuu kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara, hilo litakua jambo la haraka sana, dhumuni litakua ni kupambana ili tupate uzoefu na kuiweka timu yetu katika nafasi nzuri.”
“Tukiendelea kuwa Ligi Kuu kwa msimu utakaokuja, hapo ndipo tunaweza kuzungumza mengine, lakini ni mapema mno kusema lolote kubwa kwa sasa, zaidi ya kuhakikisha tunakwenda kupambana na kuiwezesha timu yetu inakua sehemu ya timu zitakazotajwa vizuri baada ya msimu ujao.” amesema Amis Tambwe
Tambwe ndio Mchezaji anayeongoza orodha ya wafungaji bora katika Ligi Daraja la kwanza, akiwa amefunga mabao 14 hadi sasa.
Ushindi dhidi ya Pamba FC, umeifanya DTB FC kufikisha alama 65 ambazo zinaweza kufikiwa na Ihefu FC pekee yenye alama 62 katika msimu wa Ligi hiyo.
Bado michezo miwili kwa timu zote za Ligi Daraja la Kwanza ili kumazika kwa msimu wa 2021/22, hivyo Ihefu FC itawalazmika kushinda angalau mchezo mmoja ili kuungana na DTB FC kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara.