Mdee Arekebisha Kauli "Sina hizo bilioni 10 nilikuwa nafikisha ujumbe tu"



Dodoma. Hoja ya mbunge wa viti Maalumu Halima Mdee kuhusu Sh10 bilioni imeendelea kutikisa katika mitandao ya kijamii wengi wakihoji alipata wapi kiasi hicho.

Hata hivyo jana Mdee alizungumzia jambo hilo na kukanusha kuwa hana kiasi hicho kwenye akaunti yake bali amesema kwa maana ya kufikisha ujumbe kwa Serikali.

Juzi wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mdee alihoji kwanini Serikali inakosa Sh10 bilioni kwa ajili ya kupanga ardhi kwenye vijiji wakati yeye na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wanazo katika akaunti zao.

Katika mchango wake mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Kawe, alionyesha kusikitishwa na Serikali inaposhindwa kutoa kiasi cha Sh10 bilioni ambazo zingewezesha kupima vijiji 750 kwa mwaka lakini ikatoa Sh1.4 bilioni zinazokwenda kupima vijiji 100.


Amesema mawaziri wameacha kufanya shughuli zao za msingi wanaingia katika kwenda kutatua migogoro na kwamba migogoro hiyo wanaizungumza leo ni mwaka wa 15.

“Halafu mnatuambia katika hotuba zenu kuwa mnapiga maziara, hizo ziara mmepiga nyie wakubwa tangia tumeanza kutatua migogoro ya ardhi hivi mmetumia shilingi ngapi,”alihoji.

Halima amesema kwa akili yake ya kawaida migogoro ya ardhi inatumika kama dili alilosema la kimtindo na kuacha shughuli za kufanya kwa sababu haamini kama wanakosa Sh10 bilioni.


“Pamoja na uzoefu wake Lukuvi anakosa Sh10 bilioni mimi ninayo uhakika Lukuvi kwa uzoefu wake kwenye akaunti yake hakosi Sh10 bilioni, anakosaje Sh10 bilioni ambayo hata mimi ninayo,”alihoji.

Baada ya kauli yake, yaliibuka maoni kupitia kwenye mtandao wa twita wengi wakimponda kwa kauli yake hasa kwenye kiwango cha fedha alichodai kuwa nacho.

Katika mtandao huo mtu aliyejitambulisha kwa jina la Clement Manang’ ambaye aliandika ‘hongera kukaa na dola kumuumiza Mbowe, malipo yapo’.

Aneth Stanley aliandika, my dear, unaweza kuwa na hoja nzuri tu, lakini hoja zako zinakosa uhalali mbele za umma kwa kuwa upo ndani ya bunge kinyume cha sheria, kwanza safisha hatia zako ndipo uketi useme unatetea nchi.

Kwa upande wake Robison Mwakalinga aliandika kuwa, siku ya uchaguzi mkuu ulipiga kelele kuwa umekamata kura feki, kumbe na wewe ni wa mchongo, tayari umekabana ka10 bilioni ka mchongo.

Akitoa ufafanuzi jana kuhusu kiasi hicho, Mdee leo amesema kauli yake ya kiasi hicho haikuwa kweli kwamba ana fedha isipokuwa alitumia lugha hiyo kuonyesha msisitizo kwa Serikali kama ina nia ya kupunguza au kumaliza migogoro.

“Ni kweli nilisema, lakini kwa namna nyingine watu wasingenielewa bali nilikuwa natumia njia hiyo kufikisha ujumbe kwa Serikali, hivi katika usawa huu mtu uwe na kiasi hicho si mambo yatakuwa mazuri sana,ule ulikuwa utani,” alisema Mdee akiwa nje ya ukumbi wa bunge.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad