Wizara ya Afya imesema kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa wa UVIKO-19 kutoka wagonjwa 8 katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili hadi kufikia wagonjwa 32 katika wiki ya nne ya mwezi huo, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kuwa na visa vya watu 70 waliothibitika kuwa na ugonjwa huo.
Katika taarifa ya Mganga Mkuu wa serikali Dkt Aifello Sichalwe, imeeleza kwamba idadi ya wagonjwa walioko Dar es Salaam ni sawa na asilimia 87.5 ya visa vyote huku mkoa wa Arusha ukiwa na visa 6, Kilimanjaro wawili, Morogoro mmoja na Mwanza ina mgonjwa mmoja pekee.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa kuanzia mwezi Aprili hadi Mei 4 mwaka huu, hakuna kifo chochote kilichoripotiwa kutokea kutokana na ugonjwa huo na katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa wawili walilazwa kutokana na ugonjwa huo na wote walikuwa hawajachanja.