Rais wa Heshima wa klabu ya Simba Mohammed Dewji kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram amesema miaka 5 iliyopita ya klabu ya Simba imekuwa ya Mafanikio na anajivunia kuwekeza ndani ya klabu hiyo. Pia ameahidi kurekebisha maeneo yenye madhaifu.
“Kwa ujumla miaka 5 iliyopita imekuwa ya mafanikio kwa Simba. Bajeti iliongezeka mara 5, tulishinda makombe mengi ya ndani na tuliweka alama kimataifa kwa kufika robo fainali tatu za michuano ya Afrika. Najivunia kuweza kusema tupo katika orodha ya vilabu bora 12 Afrika. Hii imekuwa mara ya kwanza Simba kuwa na mwendelezo mzuri katika miaka 86 ya historia yetu. Hakuna kurudi nyuma, tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna madhaifu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea” Ameandika Mohammed Dewji
Kauli ya Mo inafuatia siku chache baada ya klabu ya Simba kuvuliwa ubingwa wa michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Yanga SC kwa kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali. Yanga wanahitaji alama 3 tu kwenye michzo 4 iliyosalia iliwatangazwe kuwa mabingwa wa Tanzania bara msimu huu ambapo watakuwa wamewavua ubingwa Simba.
Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita Tangu Mohammed Dewji alipoingiwa kama mwekezaji kwenye klabu ya Simba, timu hiyo imeshinda jumla ya makombe 12 ikiwemo ubingwa wa Ligi Tanzania bara mara 4, ASFC mara 3 ngao ya Jamii mara 4 na michuano ya Mapinduzi mara 1.