SIKU moja baada ya uongozi wa Simba na winga Bernard Morrison kupeana mkono wa kwaheri, Yanga wamemkaribisha mchezaji huyo raia wa Ghana ambaye kabla ya kutua Msimbazi alitokea kwao.
Morrison ambaye mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu, lakini tangu juzi ilitangazwa hatakuwa miongoni mwa wachezaji watakaomalizia mechi zilizobaki za Ligi Kuu pamoja na ya jana ya Kombe la Azam dhidi ya Pamba.
Miongoni mwa sababu zinazodaiwa kumwondoa kikosini ni mwenendo wa kiwango chake, kutoroka kambini, utovu wa nidhamu, kuchagua mechi za kucheza na kuwa na mawasiliano ya karibu na watu wa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said alisemahakuna mchezaji mzuri ambaye hawatatamani kuwa naye kikosini kama alivyo Morrison.
Alisema kwenye Ligi Kuu msimu huu hakuna winga mwenye ubora na uwezo kama Morrison ambaye ameonekana kutofiti ndani ya kikosi cha watani zao Simba hadi kuamua kuachana naye.
“Morrison ni bonge la winga, nimeona wamemtakia kila lenye heri aendako.Yanga tunamkaribisha aje apumzike tu huku kwetu wala hatuna shida,” alisema Hersi japo hakutaka kuweka wazi mazungumzo yao na winga huyo kutaka kurejea tena Yanga.
Hersi alimkaribisha Morrison katika mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma na kushinda mabao 2-0