Mpango wa Nchi za Magharibi Kuanzisha NATO Ya Dunia Nzima

 


Katika hali ambayo suala la uwanachama wa nchi mbalimbali hasa Ukraine katika Jeshi la Nchi za Magharibi NATO limeitumbukiza dunia kwenye mgogoro wa kimataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ameona kama hiyo haitoshi na hivi sasa amezungumzia wajibu wa kuweko mkataba wa NATO ya dunia nzima.


Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uingereza, Liz Truss, amesema hayo katika kikao kisicho rasmi cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa NATO kilichofanyika mjini Berlin Ujerumani.  Aidha amesema, usalama wa barani Ulaya utazidi kuimarika iwapo Finland na Sweden zitajiunga na NATO lakini suala muhimu leo ni kuelekeza fikra zetu kwenye kuunda NATO ya dunia nzima kwani sambamba na NATO hiyo kulinda usalama wa ukanda wa Ulaya, itaweza kulinda pia usalama wa nje ya bara hilo kama wa nchi za Bahari ya Hindi na Pasifiki.


Liz Truss ametaka kutanuliwa eneo la NATO katika hali ambayo kabla ya hapo China na Russia zilikuwa zimepinga vikali mno suala la kujiingiza NATO katika maeneo ya nchi hizo zikisisitiza kuwa jambo hilo litazidi kuhatarisha usalama wa dunia.


Jeshi la Nchi za Magharibi NATO liliundwa katika muongo wa 1940 huko Washington DC nchini Marekani. Hadi hivi sasa Marekani na nchi za Ulaya na za pembeni ya ukanda huo zimeshapewa uanachama katika jeshi hilo. Nchi za NATO zimekula kiapo kuwa, wakati mwanachama yoyote wa jeshi hilo atashambuliwa, basi nchi zilizobakia zitamsaidia kwani shambulio hilo litakuwa ni sawa na kushambuliwa wanachama wote wa NATO. Jeshi hilo la nchi za Magharibi liliundwa wakati vilipokuwa vimepamba moto vita baridi baina ya nchi za Magharibi na Muungano wa Kisovieti.


Baada ya kubadilika siasa za dunia na kuvunjia mfumo wa kambi mbili kulikokuwa na maana ya kumalizika vita baridi, NATO nayo  ilibadilisha siasa zake kwa kiasi fulani. Miongoni mwa mabadiliko makubwa ya siasa za jeshi hilo ni kujitanua upande wa mashariki mwa dunia na kujizatiti kijeshi katika mipaka ya nchi mahasimu wa Ulaya yaani Russia na China. Matokeo yake ni kuwa nchi kama Poland, Hungary na Czech zilijiunga na Umoja wa Ulaya na NATO.


Kwa kweli lengo kuu la nchi za Magharibi linaonekana wazi kuwa ni kutaka kuidhibiti Russia na kujitanua zaidi upande wa Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Sasa hivi nia na madhumuni ya nchi hizo za Magharibi ni kuudhibiti ulimwengu wote hasa kutokana na sisitizo hilo la waziri wa mambo ya nje wa Uingereza la kutaka NATO iwe ya dunia nzima. Nchi za Magharibi hazifichi hata kidogo nia yao ya kutaka kuzivunja nguvu nchi wapinzani wao hasa China na Russia.


Sasa hivi nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinaendesha kampeni kubwa ya kuonesha kuwa Russia ni tishio lisilovumilika kwa usalama wa dunia. Inaonekana wazi kuwa kazi kuu ya hivi sasa ya NATO ni kukabiliana na muundo mpya wa kambi za dunia na hasa baada ya kutoka udhibiti wa mambo ya nchi za ulimwengu huu mikononi mwa madola ya Magharibi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad