MPAPASO WA MASAU BWIRE: Simba na Yanga dakika 90 tu mengine achaneni nayo



UTASHI na fikra zangu, Simba na Yanga zinapokutana katika mchezo wowote ule iwe wa ligi au bonanza mara nyingi matarajio ya wengi katika matokeo baada ya dakika 90 huwa tofauti. Lakini, pia ufundi na ubora wa wachezaji mahiri na nyota wa timu hizo zinapokutana unaweza usionekane, wakacheza hovyo kabisa na kushindwa kuzisaidia kupata ushindi.

Ni mchezo ambao huwa na mihemko mingi kwa wachezaji, mabenchi ya ufundi, viongozi na hata mashabiki kutokana hasa na kutambiana na kudozoana huku kila upande ukihofia kuzomewa endapo watafungwa na mtani, japo siku za karibuni na hata sasa utani kama unatoweka na badala yake uhasama na uadui unashika kasi.

Utabiri wa kiufundi na hata ule wa kienyeji timu hizo zinapokutana kuwa nani anaweza kuibuka mshindi huwa ni mgumu kwani mara kadhaa tumeshuhudia aliyedhaniwa ndiye ikawa siye. Ubora au udhaifu wa timu mojawapo katika msimu wa ligi zinapokutana huwa sio kigezo cha kushinda au kushindwa. Hali huwa tofauti na aliyeonekana dhaifu anaweza kuwa bora kuliko aliyeonekana bora.

Kutokana na mazingira hayo, Simba inapokutana na Yanga binafsi huwa sipendi kujadili kiufundi kwamba, ubora wa kikosi, wachezaji au benchi la ufundi la timu fulani unaweza kusababisha timu hiyo kupata ushindi.


 
Simba na Yanga ni timu zenye mashabiki wengi. Zinapokutana mashabiki wake hujaa uwanjani hali ambayo huongeza hamasa na ushindani. Huufanya mchezo kuwa mgumu zaidi kwa pande zote. Kila mmoja akijitahidi kuonyesha ufundi na ubora wa kulisakata kabumbu mbele ya mashabiki wake na kuusaka ushindi kwa nguvu na jasho jingi.

Yapo mambo kadhaa yasiyo ya kawaida ambayo mara kadhaa zinapokutana hujitokeza na kuupunguzia uungwana mchezo huo wa kiungwana ambayo kama itawezekana, tushirikiane katika kuyakemea ili yasijitokeze.

Kumekuwepo na vitendo vya kishirikina na uchawi wa hadharani kabla na wakati wa mchezo - vitendo ambavyo kikanuni haviruhusiwi. Vinadharirisha na kurudisha nyuma maendeleo ya soka. Kanuni ya 41 (5)(5), 45 (2)(4), 46 (4), 47 (2), 47 (30) za Lgi Kuu toleo la 2021 zinakataza vitendo vya kishirikina na uchawi kabla na wakati wa mchezo.


Lakini kanuni hizo zimeelekeza adhabu kwa yeyote awe mchezaji, kocha, klabu na shabiki atakayefanya vitendo vya kishirikina na uchawi ikimaanisha haramu na marufuku kushiriki ushirikina na uchawi hadharani katika soka. Inawezekana wengi hawajui kuwa ushirikina na uchawi umezuiwa kwenye soka ndio maana wanafanya hadharani bila hofu yoyote. Pia wapo wanaojua kuwa kufanya hivyo ni kosa kikanuni, lakini wanafanya makusudi kwamba liwalo na liwe.

Kupitia safu hii niwakumbushe kwamba ni kosa na adhabu yake ni kali ukibainika ukiturutumba kwenye soka kabla na wakati wa mchezo. Mchezaji atakayebainika kufanya kitendo chochote chenye kuonyesha imani za kishirikina na uchawi hadharani au kitakachobainishwa kwa ushahidi mwingine atafungiwa michezo isiyopungua mitatu na faini kati ya Sh500,000 na 2,000,000.

Kocha akibainika kushiriki ushirikina na uchawi atafungiwa michezo isiyopungua mitatu na faini ya kati ya Sh1,000,000 na 10,000,000. Kiongozi wa ngazi yoyote anayebainika akifanya vitendo vyenye kuashiria imani hizo anaafungiwa kwa miezi sita na faini ya kati ya Sh1,000,000 mpaka 10,000,000. Shabiki anayebainika kufanya vitendo hivyo anafungiwa kuingia uwanjani kwa kati ya miezi mitatu na isiyozidi 12.

Klabu ikibainika kushiriki ushirikina na uchawi itatozwa faini ya kati ya Sh1,000,000 na 10,000,000. Kwa kuwa vitendo vinavyoashiria ushirikina na uchawi vimekatazwa kikanuni na ni vya aibu, vinadharirisha soka na kulifanya lisiendelee, adhabu hizo kwa mujibu wa kanuni zitolewe kwa yeyote atakayebainika na atangazwe hadharani.


 
Simba na Yanga ni timu kubwa Afrika zinapokutana katika derby inatazamwa na watazamaji wengi barani humu. Wanapofanya mambo meusi ya kishetani wanajidharirisha wao, soka na pia wanaidharirisha Tanzania. Tusifumbie macho jambo hilo. Ikitokea tu kuanzia mchezo wa leo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) waadhibiwe. Eneo jingine linalopaswa kutazamwa na kuchukuliwa hatua kwa viongozi na mashabiki wa timu hizo zinapokutana uwanjani ni vurugu. Kumekuwa na kawaida shabiki wa upande mmoja akikosea akaelekea upande walikoketi mashabiki wa timu pinzani hupigwa na kuchaniwa nguo na jezi aliyoivaa huo sio uungwana ni uhuni na udharirishaji. Hatua zichukuliwe.

Lakini pia kumekuwepo na kawaida japo sio mara kwa mara timu hizo kujadili na wakati fulani kuwakataa waamuzi waliopangwa na mamlaka. Mbaya zaidi wanajadili na kulalamika mitandaoni. Hilo pia halina afya kwa maendeleo ya mpira. Wasiwatie hofu waamuzi wawaache wafanye kazi yao kwa mujibu wa sheria. Katika mchezo wa leo unaowakutanisha wakongwe hao wa Kariakoo katika Uwanja wa CCM-Kirumba, Mwanza mashabiki wa soka tunahitaji na tunatarajia kushuhudia kandanda safi kutoka kwa wachezaji wazoefu, mahiri na wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira kwa timu zote mbili.

Binafsi niwaombe waamuzi walioaminiwa kuchezesha mchezo huo kuwa makini na kuzingatia sheria ili isiwepo timu ya kulalamikia uamuzi wao baada ya dakika 90. Mshindi atokane na uwezo na si vinginevyo.

Pia nimpongeze mapema mshindi wa mchezo huo kwa kufanikiwa kushinda na kucheza fainali ya ASFC msimu huu. Nimpe pole atakayefungwa akubaliane na matokeo, ajipange kwa msimu ujao huenda akafika mbali zaidi ya alipoishia msimu huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad