Kocha Mkuu wa APR ya Rwanda, Mohammed Adil Erradi.
INAELEZWA kwamba, Kocha Mkuu wa APR ya Rwanda, Mohammed Adil Erradi, ametua Dar kimyakimya kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mabosi wa Simba huku akiwa ameomba ruhusa ya mapumziko katika klabu yake.
Simba imekuwa katika kipindi cha kufanya mabadiliko makubwa ndani ya timu hiyo kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri ikishindwa kutetea mataji yake yote ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, huku ikibeba Kombe la Mapinduzi.
Tayari Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji ameweka wazi kufanyika uamuzi mgumu klabuni hapo baada ya kufungwa na Yanga 1-0 na kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Spoti Xtra linafahamu kuwa, Simba imemleta nchini kocha huyo kabla ya mchezo dhidi ya Yanga na kumficha jijini Dar kwa ajili ya mazungumzo ya kujiunga na timu hiyo ambapo alitua Dar Ijumaa na kufichwa kwa takribani siku tatu.
Kiongozi mmoja wa APR ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Adil ameondoka Rwanda tangu Ijumaa, ametuambia anakwenda likizo ya kupisha ratiba ya mechi za timu za taifa, lakini kwa udukuzi wetu tunafahamu kwa Simba ndiyo wamemuita.
“Huku hakuna ambaye amemtafuta kumuuliza kwa sababu ana mkataba wa miaka mitatu na APR.
“Tunachofahamu ni kwamba Simba ndiyo wamemuita kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo, hakwenda Mwanza maana makubaliano yao ni mazungumzo yatafanyika Dar.”
Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuzungumzia ishu hiyo ya kocha, alisema: “Suala hilo siwezi kusema kama lipo au halipo kwa sababu bado halijafika kwangu.
“Kuhusu ishu ya Pablo, ni kweli hajafikia malengo kwa sababu hatujafuzu nusu fainali ya michuano ya kimataifa wala kutetea ubingwa wa ligi, hivyo tunasubiri ripoti yake.
“Katika hiyo ripoti, tutafahamu nini kimesababisha kushindwa kufikia hayo malengo, baada ya hapo ndipo itafahamika uamuzi utakaochukuliwa.”