KLABU ya Yanga imeivua rasmi Simba SC ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Bao pekee la Yanga kwenye mchezo huo lilifungwa na Feisal Salum dakika ya 25 baada ya kupiga shuti kali la umbali mrefu lililomshinda kipa, Beno Kakolanya na kutinga wavuni.
Simba waliokuwa mabingwa watetezi walitwaa kombe hilo mwaka jana baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Simba kucheza hatua ya nusu fainali, huku mbili kati ya hizo ikiwa imeshinda kombe mara mbili mfululizo mwaka 2020 waliposhinda 2-1 mbele ya Namungo na mwaka 2021 walipoibuka na ushindi wa 1-0 mbele ya Yanga.
Mchezo huu uliochezeshwa na mwamuzi Ahmed Arajiga, ulikuwa na presha kubwa kwa timu zote mbili, Yanga ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi mbele ya Simba, dakika ya tisa baada ya Fiston Mayele kupiga shuti kali lililookolewa na kipa Beno Kakolanya na kuwa kona.
Yanga walirudi tena katika lango la Simba katika dakika ya 10 baada ya walinzi wa Simba kufanya faulo na mwamuzi kutoa pigo la mpira wa kutengwa uliopigwa na Djuma Shaaban na kwenda nje ya lango.
Dakika 45 za kwanza zilihitimika Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0, kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Pablo Franco kufanya mabadiliko kwa kumtoa Thadeo Lwanga na nafasi yake kuchukuliwa na Larry Bwalya.
Yanga walikaribia kupata bao la pili katika dakika ya 55 baada ya Mayele, kupiga shuti kali lililookolewa na Kakolanya na kuwa mpira wa kurusha.
Dakika ya 59, nyota wa Simba, Kibu Denis na Kibwana Shomari waligongana na kupasuka usoni walipokuwa wakigombea mpira wa krosi uliopigwa na Pape Sakho.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, alilazimika kufanya mabadiliko katika dakika ya 63 baada ya Kibwana kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake ikachukuliwa na Farid Musa.
Yanga walifanya mabadiliko mengine katika dakika ya 67 kwa kumtoa Heritier Makambo nafasi yake ikachukuliwa na Crispin Ngushi ili kwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.
Kocha wa Simba, Pablo alifanya mabadiliko mengine dakika ya 75, kwa kuwatoa Kibu Denis, aliyeshindwa kuendelea na mchezo na Mzamiru Yasin nafasi zao zikachukuliwa na Meddie Kagere na Yusuf Mhilu ili kutafuta bao la kusawazisha.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ndipo kocha wa Yanga, Nabi alipofanya mabadiliko mengine dakika ya 82 kwa kumtoa mfungaji wa bao, Feisal na nafasi yake ikachukuliwa na Zawadi Mauya ili kuimarisha safu ya ulinzi.
Dakika ya 86 Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Jimmyson Mwanuke na nafasi yake ikachukuliwa na Erasto Nyoni, mabadiliko ambayo hayakuleta faida kwani hadi dakika 90 zinatamatika walikubali kichapo cha bao 1-0.
Ushindi huo ni kisasi kwa miamba hiyo ya Jangwani hivyo wanatinga hatua ya fainali kumsubiri mshindi baina ya Azam FC na Coastal Union ambao wanashuka kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Fainali ya Kombe la Shirikisho inatarajiwa kuchezwa Julai 2, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.