MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amesema kuwa kiungo Mghana, Bernard Morrison ni bonge la mchezaji, na wanatamani awepo katika kikosi chao msimu ujao.
Kauli hiyo imekuja baada ya tetesi nyingi kuzagaa za kiungo huyo kurejea katika timu yake ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao.
Tetesi hizo za kurejea Yanga zimekuwa nyingi kutokana na kuwepo katika orodha ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Mwakalebela alisema kuwa hakuna timu ambayo isingependa kummiliki Morrison katika kikosi chake kutokana na kiwango bora alichonacho.
Mwakalebela alisema kuwa shida ya kiungo huyo ni nidhamu pekee, lakini ndani ya uwanja yupo vizuri kutokana na kiwango kizuri alichonacho ambacho kinaipa timu matokeo mazuri ya ushindi muda wowote katika mechi.
Aliongeza kuwa hatima yake ya kurejea Yanga, ngumu kuiweka wazi kutokana na mkataba wake alionao katika timu yake ya Simba.
“Nisingependa kulizungumzia suala la Morrison kurejea Yanga, lakini ni mchezaji mzuri atakayekupa matokeo ya ushindi muda wowote akiwepo uwanjani kutokana na kiwango bora.
“Ana nafasi ya kucheza katika kikosi chetu kama akirejea tena Yanga, kiukweli Morrison ni mchezaji ambaye kila timu ingetamani kuwa naye.
“Shida yake kubwa ni nidhamu pekee, hivyo tusubirie mwishoni mwa msimu kila kitu kitajulikana kipindi ambacho mkataba wake utakuwa umemalizika ndani ya Simba,” alisema Mwakalebela.
Yanga iliingia katika mgogoro mzito na kiungo huyo hadi kufikia hatua ya kumpeleka katika Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Kimichezo (Cas) ambako Morrison alishinda kesi na kuruhusiwa kuichezea Simba.
Timu hiyo ilifikia hatua ya kwenda Cas wa kile kilichoelezwa kusaini Simba akiwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja huku yeye akidai alisaini mkataba wa miezi sita siyo miaka miwili kama Yanga walivyodai.
Kwa upande wa Simba, tayari hapo jana walitangaza kuachana na mchezaji huyo mwenye rekodi ya utovu wa nidhamu na sasa si mchezaji wao tena hivyo anaweza kujiunga na timu yeyote itakayomuhitaji kwa mujibu wa sheria na kanuni za FIFA.
Morrison alijiunga na Simba kutokea Yanga Agosti 8, mwaka 2020 katika usajili ambao ulizua mjadala mkubwa.