KWA kuweka kumbukumbu sawa ni kwamba Faustina Charles Mfinanga almaarufu Nandy; au Nandera amezaliwa Novemba 9, 1992 mjini Moshi, Kilimanjaro nchini Tanzania.
Nandy alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 6 na alipofikisha umri wa miaka 15, alijiunga na kwaya ya shule, hatua ambayo ilimsaidia kuboresha umahiri wake wa kuimba. Baadaye, aliyekuwa mwandani wake, Ruge Mutahaba; Mtendaji Mkuu wa Tanzania House of Talent (THT) alimchukua na kuikuza sanaa yake.
Wakati wake huko THT, alikutana na producer Emma The Boy ambaye alifanya kazi naye kwenye wimbo wake wa kwanza wa Nagusagusa mwaka 2016.
Awali mwaka 2015, Nandy alikwenda kushiriki Shindano la Tecno Own The Stage nchini Nigeria na kuibuka mshindi wa nafasi ya pili.
Nandy akiwa na mpenzi wake Billnass.
Mwaka 2017, aliachia ngoma yake ya One Day ambayo ilitamba na kumpa fursa ya kuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki kwenye jukwaa la Coke Studio Africa.
Baada ya hapo, Nandy alianza kutoa ngoma moja baada ya nyingine na sasa ni mmoja wa wanamuziki bora wa kike Afrika Mashariki na Kati.
Baadhi ya nyimbo zake bora ni pamoja na Leo Leo, Number One, One Day, Kivuruge, Aibu, Nibakishie, Hazipo, Acha Lizame, Ninogeshe, Kiza Kinene, Subalkheri, Nigande, Bado, Nimekuzoea, Siwezi na nyingine kibao.
Mwaka wa 2020, Nandy alitangaza rasmi kuwa kwenye uchumba na rapa Billnass au Nenga ambapo ndoa ni Juni, mwaka huu.
IJUMAA SHOWBIZ imekaa kwenye mahojiano maalum (exclusive) na Nandy ambaye anafunguka juu ya ishu mbalimbali;
IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi?
NANDY: Poapoa.
IJUMAA SHOWBIZ: Umesema kuwa akaunti yako ya instagram ni nusu ya mafanikio yako, unamaanisha nini?
NANDY: Ni kweli akaunti ni nusu ya mafanikio yangu kwa sababu imebeba vitu vingi vya muhimu. Kwanza ndiyo akaunti ambayo inaniingizia kipato. Mfano; kazi zangu nyingi za muziki huwa naposti pale, matangazo pia, lakini vilevile mashabiki wangu sitaki kuwapoteza.
IJUMAA SHOWBIZ: Ilikuwia ugumu kiasi gani kipindi umepoteza akaunti yako?
NANDY: Iliniwia vigumu sana kwa sababu nilikuwa nashindwa kufanya kazi zangu na za watu pia na asikwambie mtu nilikuwa sina furaha hadi iliporudi.
IJUMAA SHOWBIZ: Billnass ni mtu ambaye alikuwa tayari kukuachia akaunti yake uitumie endapo tu kama yako haitarudi, unalizungumziaje hili?
NANDY: Binafsi namshukuru sana na nampenda sana kwa sababu yeye ni miongoni mwa watu walipambana kuhakikisha akaunti yangu inarudi.
IJUMAA SHOWBIZ: Kuna tetesi kwamba ule wimbo wako wa Siwezi ni historia yako ya kweli ambayo umewahi kuipitia huko nyuma, hili lina ukweli kiasi gani?
NANDY: Maumivu ya mapenzi hakuna mtu ambaye hajawahi kuyapitia, binafsi nimewahi kuumizwa na mapenzi, lakini sikufikia hatua mbaya labda ya kutaka kujidhuru.
Kwa hiyo naweza kusema Siwezi nimeiimbia jamii kiujumla ndiyo maana unaona hata mapokezi yake yamekuwa makubwa na kuna baadhi ya watu walionesha hisia zao za kuumizwa waziwazi.
IJUMAA SHOWBIZ: Niliona ulimposti Gigy akiimba wimbo wako wa Siwezi kwenye akaunti yako, vipi mmeshayamaliza?
NANDY: No comment.
IJUMAA SHOWBIZ: Mitandao ya kijamii ina msaada gani kwenye kazi yako ya muziki na maisha yako kiujumla?
NANDY: Inanisaidia vitu vingi sana kwanza kunijenga kiroho na kimwili kwa sababu mara nyingi huwa napoteza muda wangu mitandaoni kuangalia mafundisho mbalimbali ya dini ambayo hunisaidia sana kiimani. Pia ndiyo sehemu ambayo huwa natoa aidia mbalimbali za nyimbo zangu.
IJUMAA SHOWBIZ: Ni kweli una mimba kama watu wanavyosema mitandaoni?
NANDY: (Anacheka) jamani sina mimba na kama ningekuwa nayo mngekuwa mmeshaiona ila kuna kipindi huwa nanenepa sana hadi tumbo huwa linakuwa kubwa hapo ndiyo watu wanaanza kusema nina mimba.
IJUMAA SHOWBIZ: Maandalizi ya ndoa au harusi kwa upande wako yakoje?
NANDY: Maandalizi yapo vizuri namshukuru Mungu, vikao vimeshaanza kufanyika, nina imani kila kitu kitakuwa sawa.
IJUMAA SHOWBIZ: Mfano ikatokea Billnass amekusaliti utachukua hatua gani?
NANDY: Hajawahi kunisaliti kwa hiyo bado sijajua nini cha kufanya, ikitokea ndiyo tutajua hapohapo.
IJUMAA SHOWBIZ: Billnass ni mtu wa aina gani?
NANDY: Ni mwanaume ambaye kiukweli hana mambo mengi, nikikuambia tangu tumeanza uhusiano sijawahi kukuta hata meseji za wanawake huwezi kuamini, kwa hiyo naweza kusema yupo tofauti sana na wanaume wengine.
IJUMAA SHOWBIZ: Miezi kadhaa iliyopita mama pamoja na dada yako, walifanya interview na kuonekana kama hawapendi uolewe na Billnass na sasa tunaona mnakaribia kufunga ndoa, hili nalo unalizungumziaje?
NANDY: Siyo kama walikuwa hawapendi mimi niolewe na Billnass ila walikuwa wanachukia yale mambo yaliyokuwa yanaendelea mitandaoni baina yetu. Hivyo wao kama wazazi walihitaji hatua f’lani za kifamilia azifanye na Mungu mwema alishazifanya ndiyo maana mnaona tunakaribia kuwa mke na mume halali.
IJUMAA SHOWBIZ: Umeshawahi kufikiria kuingia kwenye siasa kama ilivyo kwa mastaa wengine?
NANDY: Mmmh! Siasa naipenda sana, napenda jinsi ambavyo viongozi wetu wanafanya kazi nzuri tena kwa kujituma sana, ila kwa upande wangu bado sijawaza kuwa mwanasiasa.
IJUMAA SHOWBIZ: Unaizungumziaje ishu ya mastaa wengi kutojenga ilihali wanaonekana wakifanya starehe?
NANDY: Nadhani tusiwalaumu pale ambapo inaonekana wamechelewa kujenga kwa sababu huwezi kujua anapitia mambo gani, kuna wengine wao ndiyo kila kitu kwenye familia zao, asomeshe ahudumie wazazi, ndugu sasa unakuta muda mwingine anazidiwa hadi anachelewa kujenga.
IJUMAA SHOWBIZ: Ni kweli kwamba lile duka la Nenga Tronix ni lako na siyo la Billnass?
NANDY: Unajua watu huwa wanazungumza vitu ambavyo hawavijui kabisa, biashara anayoifanya kwa sasa mume wangu mtarajiwa ni nguvu zake mwenyewe na ni kazi aliyoanza nayo muda mrefu sana, hivyo najivunia yeye kwa kweli.
IJUMAA SHOWBIZ: Huwa unajisikiaje watu wanavyosema Billnass analelewa na wewe?
NANDY: Siwezi kujisikia vibaya kwa sababu hayo yanayosemwa siyo kweli, anapambana na jitihada zake zinaonekana
IJUMAA SHOWBIZ: Kuna tetesi kuwa na wewe ulitengeneza shepu yako kwa sababu mwanzo haikuwepo…
NANDY: Jamani! Ngoja niwaambie siri ya shepu yangu, mimi nafanya sana mazoezi ya squat na siyo vinginevyo.
IJUMAA SHOWBIZ: Kati ya muvi na muziki, tutegemee kukuona zaidi wapi?
NANDY: Tegemeeni kuniona kotekote kwa sababu tamthiliya zimeniongezea mashabiki wapya hivyo siwezi kusema nitaacha kuigiza.
IJUMAA SHOWBIZ: Kuna wasichana wengi mtaani ambao wana vipaji vya kuimba, lakini wengi wao wanashindwa kutoka na dhana iliyopo kwamba ili binti atoboe kimuziki, basi inatakiwa atoe rushwa ya ngono, wewe kama msichana uliyefanikiwa kisanaa unawashauri nini?
NANDY: Unajua ishu ya kutoa ngono ili utoboe mimi huwa naona ni mihemko yao wao wenyewe kwa sababu ukijitambua nakusimamia kile unachokitaka hakuna mtu atakayekusumbua. Na kama una kipaji kwa nini uhangaike kutoa rushwa ya ngono? Binafsi nawashauri wapambane wasijirahisishe kama Mungu kakuandikia riziki yako ipo tu hata hata iweje.