Nchemba, Shigongo wavutana nchi kurudi uchumi wa chini




Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo
MVUTANO umeibuka bungeni baina ya Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kuhusu nchi kuporomoka kutoka uchumi wa kati hadi uchumi wa chini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mvutano huo umeibuka leo Jumatatu tarehe 9 Mei 2022 baada ya Shigongo kueleza bungeni hapo kuwa taifa limeporomoka kutoka uchumi wa kati hadi uchumi wa chini tofauti na miaka miwili iliyopita.

Mbunge huyo amesema pato la mtu mmoja mmoja limeshuka hadi Dola za Marekani 976 na hivyo kuifanya Tanzania kukosa sifa zinazoifanya nchi kuwa uchumi wa kati.

“Nchi yetu Tanzania miaka miwili iliyopita tulisheherekea tukashangilia kwa pamoja kupanda mpaka uchumi wa kati, GDP ya Taifa ilikuwa, per capita income ikaongezeka na hivyo tukasheherekea kwamba nchi yetu inakwenda vizuri.


 
“Lakini ninavyozungumza na wewe hivi sasa nchi yetu imerudi tulipokuwa, ‘per capita income’ imeshuka hadi dola 976, ina maana tumeporomoka chini kwasababu yeyote ile iwe covid au yeyote ile ukweli tumeporomoka,” amesema.


Wakati akieleza hayo Dk. Nchemba aliomba kuweka sawa jambo hilo na kueleza kuwa kilichoshuka ni ukuaji wa uchumi (growth rate)na si viwango vya pato la Taifa (level of income).

“Nataka niweke kumbukumbu sawa kwamba hatujarudi tulipokuwa na hii naomba isikike vizuri sana. Tulitoka uchumi wa chini tukaenda uchumi wa kati wa chini hatujawahi kurudi uchumi wa chini tena,” amesema Nchemba.


Ameongeza, “tunachozungumza ni ukuaji na si level ya uchumi. Kuna tofauti ya level of income ya nchi na growth rate.”

Amesema kilichobadilika ni kutoka ukuaji wa asilimia saba na kushuka hadi asilimia nne ya ukuaji wa uchumi “na tangu tushuke tushapanda hadi 4.9.”

Waziri huyo amesema kwa takwimu zinazokamilika za 2021 ukijumlisha wastani wanaenda asilimia tano “na kwa mwaka 2022 tunaenda asilimia 5.2 na hata wenzetu wa Benki ya dunia juzi walisema huenda tukaenda hata 5.5.”


Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango
Hata hivyo Shigongo hakukubaliana na hoja za Nchemba ambapo alieleza kuwa kigezo kinachotumika nchi kuwa uchumi wa kati ni kuwa na pato la mtu mmoja mmoja la kati ya Dola za Marekani 3033 hadi 4045 na kwamba Tanznaia ilifikia Dola 3080 ndiyo ikafika uchumi wa kati.

Alisema kwa takwimu za sasa pato la mtu mmoja mmoja limefikia Dola za Marekani 976 hivyo ni Dhahiri kuwa nchi imerudi uchumi wa chini.

“Ndiyo maana na sema tumerudi kwasababu ‘per capita’ imeshuka, hoja yangu ni kwamba kurudi nyuma sio sababu cha msingi ni kushirikiana na wabunge turudi tulikokuwa uchumi wa kati, na hili litawezekana kwa kuimarisha kilimo kwa kutafuta masoko.,” amesema Shigongo.

Shigongo ameomba TANTRADE kupewa fedha za kutosha ili iweze kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo za Tanzania badala ya kuishia kuandaa maonesho ya sabasaba.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad