Ofisi ya Msajili Lawamani Migogoro vyama vya Siasa

 


Dar es Salaam. Baada ya viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema kumtupia lawama Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuchochea migogoro ndani ya vyama hivyo, kiongozi huyo amesema ofisi yake haichochea bali migogoro hiyo inaanzia ndani ya vyama vyenyewe.


Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na Mwananchi, juu ya tuhuma za kuhusika kuchochea mgogoro ndani ya chama cha NCCR Mageuzi ambao umepamba moto huku upande mmoja ukiituhumu ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchochea mgogoro huo kwa kutambua upande ulioitisha mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho. “NCCR Mageuzi walikuwa na mkutano wao, wametualika wenyewe, tumetuma watu wa Ofisi ya Msajili, ameenda ndugu Nyahoza, bahati nzuri yanayotokea baada ya hapo ni Msajili, jamani Msajili hana nguvu kubwa sana ya kuingilia wanachama na kuunda kambi ndani ya vyama” alisema


Mei 21, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi ilimsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti (Bara), Angelina Mtahiwa kutojihusisha na shuhhuli zozote za chama hadi Mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.


Hata hivyo, Mbatia na wafuasi wake wamepinga uamuzi huo wa Baraza Kuu wakisema ulikuwa ni mkutano batili na wanashangaa kuona Ofisi ya Msajili ikishiriki kwenye mkutano huo huku ikifahamu kwamba haukuwa halali.


Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Mohamed Tibanyendela juzi alisema baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichoitishwa na Mbatia, kwamba, hawatambui mkutano wa halmashauri kuu uliofanyika Mei 21 kwa sababu haukuwepo kwa mujibu wa Katiba.


Tibanyendela alisema Kamati Kuu ililaani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia migogoro ya vyama vya siasa na tayari wameshamwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa barua na mamlaka yake ya uteuzi.


Related

wazichapaa

NCCR-Mageuzi wazichapa kavukavu

ADVERTISEMENT

Jana wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa NCCR Mageuzi Edward Simbeye alisema wanashangaa kuona Ofisi ya Msajili ikishiriki mkutano ule licha ya kuandikiwa barua kumjulisha uamuzi wa chama wa kumsimamisha Katibu Mkuu.


“Msajili anapofika pale anapaswa kuangalia, je, hiki kikao ni halali? Msajili wa Vyama ana Katiba za vyama vyote na jukumu lake ni kusimamia hivi vyama na kuona haki inatendeka na kufuata katiba zao” alisema.




Chadema yatia mguu


Akizungumzia mgogoro wa NCCR Mageuzi jana, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema umepandikizwa na kwamba Ofisi ya Msajili imekuwa ikifanya hivyo kwa kipindi cha miaka sita ya serikali ya awamu ya tano.


Mnyika alitaka vyama visiingiliwe kwa njia haramu na kutengenezewa migogoro.




Maelezo ya Mutungi


Kuhusu barua iliyoandikwa na Mbatia pamoja na ile iliyoandikwa na upande wa pili, Jaji Mtungi alisema siyo rahisi kuzungumzia suala hilo kwa sababu bado hazijafika mezani kwake, hivyo aliwataka wananchi kuwa na subira


“Ofisi ya Msajili haiwezi kufanya kazi kwa mihemko…na mara nyingi hatuongei na vyombo vya habari kuhusu vitu tunavyoviamua, sisi tunatoa maamuzi, njoo kwa msajili ukisema Mheshimiwa naomba ufafanuzi kuhusu maamuzi fulani uliyoyatoa,” alisema msajili huyo.


Malalamiko kama hayo yaliwahi kutolewa na vyama vingine kwenye migogoro yao, wakisema Ofisi ya Msajili imekuwa ikichochea migogoro hiyo badala ya kuvisaidia kuitatua ili visonge mbele.


Moja ya migogoro hiyo ni pamoja na ule wa Cuf kati ya aliyekuwa Matibu Mkuu, Maalim Seif Sahrif Hamad na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba ambapo upande wa Maalim Sief ulimtuhumu Msajili kuingilia mgogoro huo.


Aprili 10, 2017, Maalim Seif aliituhumu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ilishinikiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) ipitishe majina ya wajumbe wa bodi ya wadhamini yaliyopelekwa na upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.


“Tunajua Msajili amekuwa akiwasiliana na Rita kutia shinikizo wajumbe feki wa bodi ya udhamini ndiyo wasajiliwe,” alisema Maalim Seif.


Hata hivyo, Jaji Mutungi alikanusha tuhuma hizo akisema ofisi yake haihusiki na migogoro hiyo bali ni vyama vyenyewe na wakati mwingine hupelekeana Mahakamani kwa ajili ya utatuzi.


“Ule mgogoro wa Cuf ulikuwa ni kati ya Maalim Seif na Profesa Lipumba, mgogoro ule uliishia Mahakamani. Aliyeshinda Mahakamani ni Profesa Lipumba, kwa hiyo mimi nilisababisha, nilienda mpaka Mahakamani nikawakorofisha?” alihoji Msajili.


Chadema kimekuwa kwenye mgogoro na wabunge wake 19 wa viti maalumu ambao kimewavua uanachama hivi karibuni, hata hivyo, wabunge hao walikimbilia Mahakamani kuweka zuio la kuvuliwa uanachama wao.


Hata hivyo, Msajili alihoji kuhusika kwake kwenye mgogoro huo huku akitaka ofisi yake isihusishwe kwenye migogoro inayotokea kwenye vyama vya siasa kwa sababu hakuna uhusiano wowote.


“Chadema wana mgogoro na wabunge wake 19 ukihusisha mambo ya uchaguzi na Tume iko pale, nalo mtasema Msajili? Huo mgogoro ni wa Msajili kweli, Msajili ndiyo amesababisha?” alisema Jaji Mutungi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad