KOCHA Pablo Franco hataki utani, baada ya kuamua kuwachomoa nyota watatu katika kikosi kitakachovaana na Ruvu Shooting usiku wa leo katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku Clatous Chama na Bernard Morrison ‘BM3’ wakishtua mashabiki.
Simba inavaana na Ruvu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, bila straika wao Chriss Mugalu, Chama na Morrison waliochomolewa na Pablo kiasi cha kushindwa kuonekana kwenye mazoezi ya mwisho ya timu hiyo juzi jioni.
Wachezaji hao pamoja na Erasto Nyoni sambamba na Sadio Kanoute na Hassan Dilunga hawakuwepo mazoezini katika Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju.
Taarifa za ndani ni kwamba Pablo amewaengua BM3 na Chama tangu mchezo uliopita na Namungo na safari hii akamjumuisha na Mugalu. Mbali na wachezaji hao kukosekana mazoezini kwa sababu zilizoshindwa kuwekwa wazi na mabosi, lakini juzi Erasto Nyoni naye hakuwepo sambamba na Sadio Kanoute na Hassan Dilunga walio majeruhi.
Mwanaspoti ambalo lilifika kwenye mazoezi ya timu hiyo lilishuhudia benchi la ufundi likipambana kutoa mbinu za ushindi kwenye mechi hiyo baada ya kutoka sare ya bao 2-2 na Namungo.
Mmoja wa viongozi wa Simba, alifafanua juu ya wachezaji hao kutokuwepo mazoezini kuwa walipewa mapumziko ya siku tano na watarejea kesho Jumatatu.
“Sababu ni kwamba wana majeraha ndiyo maana kocha aliwapa mapumziko ya siku tano. Wanarejea Jumatatu na hakuna sababu zingine nje ya hizo, ikumbukwe kwamba baadhi hawakuwemo kwenye mpango wa kocha tangu mechi iliyopita na Namungo,” alisema.
TIZI LA KIBABE
Katika mazoezi ya juzi Pablo aliwapigisha tizi la kufunga mabao nyota wake akionekana akitaka kuisapraizi Ruvu, akiangalia vitu vitatu muhimu kwa timu yake kuhakikisha inapata matokeo mazuri.
Pablo alizingatia ufungaji wa mabao akiwachezesha Meddie Kagere na John Bocco na kuwachezesha mipira ya faulo - matatizo ambayo yamekuwa yakiitesa Simba msimu huu kuanzia kwenye ligi hadi kimataifa.
Kwenye mazoezi hayo mastraika hao wawili walioonekana, Bocco alifunga mabao manne huku Kagere akiingia kambani mara tatu pamoja na kutengenezewa nafasi nyingi na wenzake.
Mbali na washambuliaji hao ambao ndio walipewa kipaumbele zaidi wengine waliofunga ni Yusuf Mhilu matatu, Kibu Denis moja huku Pape Sakho akiingia kambani mara mbili.
Kwenye zoezi la upigaji wa kona ambalo pia limekuwa changamoto upande wa kushoto mipira ilikuwa inachongwa na Rally Bwalya, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, kulia ikichongwa na Shomari Kapombe, Peter Banda. Kwenye zoezi hilo ni Bocco tu ambaye aliweza kufunga mabao mawili moja kwa kichwa na mguu huku mengine yakifungwa na beki Pascal Wawa ambaye alifunga manne yote kwa kichwa. Wakati kwenye mipira ya faulo zoezi lilikuwa gumu kwa wachezaji hao kutokana na kushindwa kufanya kile alichoelekeza Pablo kwa kukosa umakini na kushindwa kuwafunga makipa watatu waliokuwa wanapokezana Beno Kakolanya, Aishi Manula na Ally Shomari.