KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema kuwa mchawi mkubwa wa timu hiyo kushindwa kufanya vyema kwenye michezo mikubwa inatokana na kikosi hicho kutokuwa na wachezaji wenye viwango bora mfululizo jambo ambalo limechangia kushindwa kufanya vyema.
Simba mpaka sasa imebaki na matumaini ya kufanya vyema katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, huku wakitolewa katika michuano ya kimataifa na kwenye ligi kuu wakiwa wana nafasi ndogo ya kutwaa ubingwa kutokana na kuachwa mbali na wapinzani wao, Yanga.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa mabosi wa klabu hiyo wanatarajia kuachana na mastaa sita wa kimataifa kwa ajili ya kufanya maboresho ya kushusha majembe mengine ya kukiongezea nguvu kikosi chao.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha Pablo alisema kuwa, Simba inahitaji kupata wachezaji wenye ubora mzuri hiyo ni kulingana na kwa sasa kushindwa kufanya vyema kwa kutamba kufanya vizuri haswa katika michezo mikubwa jambo ambalo halimpendezi.
“Imeonekana ni ngumu zaidi kwa Simba kupata matokeo mazuri katika michezo mikubwa kutokana na ubora ndani ya timu kuwa wa kawaida, tunahitaji kufanya vyema na ili iwe hivyo basi tunatakiwa kuwa na ongezeko la wachezaji bora ndani ya timu.
“Ubora wa wachezaji ni muhimu kwa Simba na hatuwezi kuwa bora katika uongozi tukasahau ubora katika timu, lazima tuweke mipango ambayo itakuwa sahihi kwa afya ya timu yetu na bado tutaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha tunafanikiwa katika mipango yetu,” alisema kocha huyo.
Stori: Marco Mzumbe na Joel Thomas