KOCHA wa Simba, Pablo Franco hajaridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake katika mechi yao waliyoshikiliwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuwaweka mahasimu wao, Yanga jirani zaidi na kombe, akisema anataka kikao kizito na wachezaji wake.
Akizungumza na Mwanaspoti Pablo alisema sare ya hiyo imemnyima raha kwa sababu wachezaji wake hawakupambana kiasi cha kutosha.
Pablo alisema kuwa timu yake haikuonyesha ubora mkubwa kwa heshima ya jina la Simba na kwamba anataka kufanya kikao na wachezaji wake kujua shida ipo wapi kabla ya kukutana na watani wao Yanga kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Mei 28, hapohapo Uwanja wa CCM Kirumba.
“Hatukuwa na mchezo bora sana, hatukucheza soka letu ambalo tunajivunia siku zote, tulikuwa katika ubora mdogo, hili sio soka ambalo Simba inatakiwa kucheza,” alisema Pablo.
“Tunahitaji kukaa na wachezaji tujue kipi kimetukuta kabla ya kukutana na Yanga, tunahitaji mabadiliko makubwa ya kiakili kama kweli tunataka kushinda hiyo mechi.”
Aidha, Pablo amesema wimbi la majeruhi wa kikosi hicho linatishia ukamilifu wa kikosi chake huku akivuta subira kujua wangapi watarejea kabla ya kukutana na Yanga.
Juzi Simba, kipa wake namba moja, Aishi Manula alikutana na masahibu ya kujikata na vioo kufuatia, moja ya kioo katika chumba cha kubadilishia nguo kuvunjwa na watoto wakiwa wanacheza nje, ambapo alilazimika kutibiwa na kuondolewa katika mchezo dakika chache kabla ya mechi kuanza.
Mbali na Manula pia beki wa kulia Shomari Kapombe aliumia sekunde chache baada ya Simba kuruhusu bao la Geita na akashindwa kuendelea na mchezo huku Mzambia Clatous Chama akiwa bado hajaweza kuwa tayari.
“Chama ni mgonjwa haya majeraha alikuja nayo akitokea Berkane, tulidhani angekaa nje kwa siku kumi lakini imekuwa wiki tatu sasa, hata ukija hotelini utamkuta anatibiwa na madaktari, leo pia tumeongeza idadi ya majeruhi wengine hii inatufanya kusubiri tuone hizi siku zilizobaki kuona kipi kitabadilika.”