TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, imeendelea na uchunguzi wa askari polisi wanne ambao wanatuhumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa huo, Leonidas Felix, alisema askari polisi hao wanatoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Geita, na kwamba uchunguzi ukikamilika watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Felix alisema katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2022, TAKUKURU Mkoa wa Geita imefanya kazi ya uzuiaji wa vitendo vya rushwa kwa kiziba mianya inayochangia uwapo wake kwa kuendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
Aidha, alisema jumla ya miradi ya maendeleo 19 katika sekta za afya, elimu, ujenzi, maji na kilimo yenye thamani ya Sh. bilioni 18.67 ilifuatiliwa. Thamani hiyo ni kwa mujibu wa mikataba ya miradi husika.
Alisema miradi 15 yenye thamani ya Sh. bilioni 18.3 ilibainika kuwa na mapungufu ya kutozingatiwa kwa vigezo na masharti yaliyoainishwa kwenye michoro na kukosekana kwa usimamizi thabiti kutoka kwa wataalamu wa halmashauri, pamoja na baadhi ya mafundi walioshinda zabuni za ujenzi kutokuonekana katika eneo la mradi na kuwaacha mafundi wasaidizi pasipo usimamizi wala maendeleo eneo la ujenzi. Baada ya ufuatiliaji huo, wahusika walishauriwa namna bora ya kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia vikao kazi.
“Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2022, tumepokea taarifa za malalamiko 75 ambapo taarifa zilizohusu rushwa ni 40 na 35 hazihusiani na rushwa, hivyo tumezitolea ushauri na kuelekeza walalamikaji mahali sahihi pa kupeleka malalamiko yao. Sekta inayoongoza kwa malalamiko ni eneo la Serikali za Mitaa 32, binafsi 10, fedha 7, elimu 8, misitu 3, sekta ya madini 3, afya 3, ardhi 3, polisi 2, mahakama 1, ujenzi 1 na zilizohusu siasa 2,” alisema.