Polisi yazingira ofisi za NCCR-Mageuzi



Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limezingira ofisi za makao makuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi zilizoko Ilala kuhakikisha hakuna shughuli zozote zinazofanyika katika ofisi hizo.

Leo Jumapili mei 22, 2022 Mwananchi imeshuhudia Polisi zaidi ya kumi wakiwa na magari mawili na silaha za moto wamezingira ofisi hizo baada ya kutokea vurugu jana kutokana na Halmashauri Kuu kumsimamisha Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia na Makamu wake upande wa Bara, Angelina Mtahiwa.

Kikao hicho cha Halmashauri Kuu kilikutana jana katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu uliopo Kurasini na kutangaza kuwasimamisha viongozi hao wawili wa chama hicho.

Katika maazimio hayo, Kikao cha Halmashauri Kuu kilichohudhuriwa na wajumbe 52 kati ya 85 waliopaswa kuwepo kilimsimamisha mwenyekiti huyo na makamu wake kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwamo kuchochea migogoro ndani ya Chama na kushawishi viongozi kujiuzulu nafasi zao.


 
Muda mfupi baada ya mkutano huo ulioongozwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu, Joseph Selasin, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Martha Chiomba akiwa ameambatana na walinzi walifika kufunga ofisi za chama hicho makao makuu huku akitangaza kuwa hakuna shughuli zitakazoendelea katika ofisi hizo hadi wiki ijayo.

Hata hivyo, baada ya ofisi hizo kufungwa baadhi ya wanachama wanaodaiwa kuwa upande wa Mwenyekiti wa Chama hicho walifika katika ofisi hizo wakitaka kuzifungua jambo ambalo lilileta vurugu kwa muda.

Baada ya ofisi hizo kufunguliwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye alizungumza na waandishi wa habari huku akidai kuwa kilichofanywa na kundi lililojipa sura ya Halmashauri Kuu ndani ya chama hicho ni uhaini.

Muda mfupi baada ya Simbeye kumaliza mkutano huo na waandishi wa habari, vurugu ziliibuka baina ya pande mbili ule unaounga mkono maamuzi ya Halmashauri Kuu na wale wanaomuunga mkono Mbatia.

Leo, Mwananchi ilipofika kwenye ofisi hizo ilishuhudia zimezingirwa na polisi huku waandishi wakizuiwa picha katika ofisi hizo.

Mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kuwa ofisi hizo zimeagiwa kufungwa mpaka Jumanne Mei 24, 2022.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad