By Noor Shija
Dodoma. Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi amesema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa azaliwe Kenya, lakini mapatano ya mipaka kati ya Uingereza na Ujerumani waliokuwa wakoloni wa eneo hili yalifanya azaliwe Tanganyika.
Profesa Kabudi alisema hayo juzi, alipokuwa akitoa mada kwenye kongamano la miaka 100 ya Mwalimu Nyerere lililohusisha uzinduzi wa taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“Nyerere alizaliwa Tanganyika kutokana na mapatano ya mipaka kati ya makoloni ya Ujerumani na Uingereza,” alisema Kabudi.
Historia hiyo alisema imo kwenye kitabu kilichoandikwa na Dk Heinz Schneppen, aliyekuwa balozi wa Ujerumani nchini Tanzania kuanzia mwaka 1993 hadi 1996.
Profesa Kabudi alikionyesha kitabu hicho kinachoitwa ‘Why Kilimanjaro is in Tanzania: Some reflections on the making of this country and its boundaries 1996’ na kitabu kingine kinachoitwa ‘Why Tanzania is where it is: Tanzania’s colonial boundaries from the Berlin Conference 1884-1885 until its independence 1998’.
“Kama si mapatano hayo eneo alilozaliwa Nyerere lilikuwa liwe upande wa Kenya,” alisema.
Alisema Tanganyika ilianzishwa na wakoloni wa Ujerumani, lakini Tanzania imeanzishwa na Waafrika wenyewe, ikiasisiwa Mwalimu Nyerere na Abeid Amani Karume kwa kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika.
Alisema uhuru wa Tanganyika ulipiganiwa kwa kujumuisha Watanzania wenye asili ya Asia na wazungu na baada ya uhuru walijumuishwa serikalini.
Profesa Kabudi alisema Mwalimu Nyerere alikuwa na mipango ya maendeleo ya muda mrefu, akitaja uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu ya Tanu kuanzisha mpango wa miaka 20 ya ujenzi wa viwanda.
“Wanaosema Serikali haina mipango ya maendeleo ya muda mrefu wanakosea, mwaka 1974 Tanu iliweka mipango ya miaka 20 kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1995 ya ujenzi wa viwanda ambao ulihujumiwa,” alisema.
Kwa upande wake, mbunge mstaafu wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka alisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanaharakati wa kimataifa wa kupigania haki za kiuchumi anayeheshimika.
Alisema Mwalimu Nyerere na Karume ni Waafrika pekee wenye sifa ya kuanzisha nchi, kwani kwingineko wanaishi kwa mipaka ya enzi ya ukoloni.
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe akieleza kuhusu uamuzi wa Mwalimu kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, alisema viongozi wana la kujifunza.
Alisema viongozi wanatakiwa kuwa na uthubutu kuamua mambo kwani kupanga ni kuchagua.
Profesa Mwamfupe alisema viongozi wanapaswa kujifunza ushirikishaji kwa kuwa jengo la makao makuu ya CCM la Dodoma lilijengwa kwa michango ya mikoa yote ya Tanzania.