RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wanaokosoa safari zake nje ya nchi wafanye tathmini kabla ya kufanya hivyo. Alisema hayo katika Ikulu ya Chamwino Dodoma wakati wa mahojiano na Ofisa Mtendaji Mkuu wa vyombo vya habari vya Azam, Tido Mhando.
Rais Samia alisema alipoapishwa kuwa Rais, safari yake ya kwanza aliifanya nchini Kenya ambako kwa kushirikiana na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta, walifanikiwa kuondoa vikwazo 64 vya kibiashara vilivyokuwapo kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Alisema kulikuwa na sintofahamu ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ikiwamo malori kuzuiwa mipakani kwa muda mrefu, kuchomwa kwa vifaranga vya kuku na mahindi kuzuiwa kutokana na madai ya kuwa na sumukuvu.
“Lakini nilipokwenda tukazungumza, tukaondosha vikwazo vile vyote, sasa hivi biashara kati ya Tanzania na Kenya imekua maradufu, na imekuwa zaidi kwa upande wetu,” alisema Rais Samia.
Baada ya kutoka Kenya alisema alikwenda nchini Uganda ambako nako kulikuwa na shida kidogo kwenye mradi wa bomba la mafuta na tatizo hilo liliondolewa na mradi unaendelea.
Alisema kisha alikwenda Umoja wa Ulaya ambako nako kulikuwa na miradi ya Tanzania iliyokwama lakini sasa inaenda vizuri.
Alisema kila anakokwenda, anakwenda na wafanyabiashara na kuwakutanisha na wenzao na kumesainiwa mikataba kadhaa ya ushirikiano kama safari ya hivi karibuni katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambako walirudi na mabilioni ya dola.
“Juzi tumerudi kutoka Marekani, tumesaini mikataba ambayo kama itatekelezwa kila mkataba karibu trilioni 11. Wafanye tathmini enzi hizo hatuendi biashara ilikuwaje ndani na sasa tunakwenda biashara ikoje. Hata huku kwenye dini yangu kwa mfano, sisi tunaambizana ‘Mguu wa kwenda Mtume kauombea,” alisema Rais Samia.
Alisema mwezi unaokuja ameshapata mialiko ya kwenda nchi nne ikiwamo Uganda, Oman na nyinginezo lakini kuna viongozi wenzake pia wanaokuja nchini akiwamo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Waziri Mkuu wa Ethiopia, jumuiya ya wafanyabiashara wa Marekani.
Rais Samia alisema kwenda kwake nje ya nchi kunafungua milango kwa wageni nchini na ndivyo maendeleo yanavyopatikana. Alisema hawezi kubaki hapa kuona watu wakilia ukata wakati hana uwezo wa kujaza mifuko yao.
“Ili kujaza mifuko yao ni kwenda kutafuta, wawekezaji waje, mifuko ya wananchi ijae na maendeleo yapatikane,” alisisitiza.