RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuondoka nchini leo tarehe 23 Mei, 2022 kuelekea jijini Accra nchini Ghana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Jaffar Haniu imeelezwa kuwa akiwa nchini Ghana, Rais Samia anatarajiwa kushiriki mdahalao wa wakuu wa nchi utakaojadili fursa zilizomo na changamoto zinazozikabili nchi za Afrika.
Pia mdahalo huo utajadili kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na matumizi ya nishati endelevu.
Imesema Rais Samia pia anatarajiwa kupokea tuzo ya mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombonu ya usafirishaji ambayo hutolewa kwa Mkuu wa Nchi iliyofanya vizuri zaidi.
“Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka katika Mkutano wa AfDB ambao kwa mwaka 2022 unafanyika jijini Accra nchini Ghana,” imesema taarifa hiyo.