Dodoma. Siku moja baada ya Gazeti la Mwananchi kuchapisha taarifa kuhusu Mariam Mchiwa (19) binti aliyelazimika kufanya kazi za ndani ili apate fedha za kujisomesha, uongozi wa Mkoa wa Dodoma umeamua kulitafutia ufumbuzi jambo hilo.
Mariam ambaye alimaliza kidato cha nne mwaka jana katika shule ya sekondari Songambele mkoani Dodoma na kupata ufaulu wa daraja la kwanza, alifikia uamuzi wa kwenda jijini Dar es Salaam kutafuta kazi za ndani kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha.
Uamuzi wa Serikali kuingilia kati unarejesha matumaini ya binti huyu kupata elimu na kujiunga na wanafunzi wenzake akiwa amechaguliwa sekondari ya wasichana Songea.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka, alithibitisha kupata taarifa kuhusu binti huyo na kuagiza afike kwenye ofisi yake kwa ajili ya kuzungumza naye na kuangalia hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa.
Jana Mariam aliwasili jijini Dodoma na kupokewa na mmoja wa watumishi wa idara ya ustawi wa jamii aliyempeleka kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa hatua zaidi na Mwananchi, hakupata taarifa zaidi ya kilichojadiliwa baada ya binti huyo kukutana na wenyeji wake.
Akizungumza kuhusu maisha ya binti huyo, kaka yake Elikana Mchiwa, alisema familia inaunga mkono mtoto huyo kusoma lakini hawana fedha za kumsomesha.
“Sisi watatu nikiwemo mimi ambaye ni mtoto wa pili hatukusoma kabisa, maisha kwetu ni magumu na mdogo wangu kasoma kwa tabu sana,” alisema Elikana.
Alisema kutokana na ari aliyokuwa nayo mdogo wao kwenye masomo walijua atafaulu kutokana na uwezo aliokuwa nao tangu shule ya msingi kwani hadi anamaliza kidato cha nne alikuwa akishika nafasi tatu za juu.
Alisema hawana uwezo hata kama wangechanga hawawezi kwani walitaka kuuza shamba ili wapate fedha za kumpeleka shule lakini wamekosa wateja wa kununua ekari moja kwa Sh50,000.
Kuhusu kwenda Dar kufanya kazi za ndani alisema familia ilimzuia lakini akajenga hoja kuwa lazima akatafute chochote cha kuanzia gharama za maisha.