MRUNDI Saido Ntibazonkiza yupo kwenye majadiliano na Yanga kuhusiana na muda wa mkataba wake mpya huku Mwanaspoti likitaarifiwa kwamba amegomea wa muda mfupi.
Staa huyo ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika msimu huu, uongozi unataka asaini mwaka mmoja lakini imeelezwa anashinikiza miaka miwili. Tayari Yanga imemalizana na wachezaji wake watatu ambao mikataba yao inamalizika msimu huu ambao ni Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari na Zawadi Mauya.
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Klabu ya Yanga, Hersi Said alipoulizwa kuhusiana na ishu ya Saido alisema Ntibazonkiza ataendelea kuwepo Yanga na suala la mkataba linazungumzika.
“Hakunaga mkataba usio na makubaliano hilo ni baina yetu kama klabu na mchezaji, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwatumikia wananchi suala la miaka mingapi? Tusubiri baada ya mambo kwenda sawa itafahamika kama ilivyo kwa wengine,” alisema.
“Hadi sasa bado ni mchezaji wetu na ndio maana anaendelea kuitumikia timu, maneno yamekuwa mengi kwasababu ni wakati wa usajili kila mmoja anazungumza kile anachojisikia kufanya. Kuna waliomuondoa kikosini na wengine wameshamsainisha hivyo muda utaongea.
“Ni mapema kukufahamisha nani na nani anaachwa kipindi hiki tukiwa bado hatujamaliza ligi. Hili litawekwa wazi baada ya msimu kuisha na kwa wachezaji walio nje ya timu bado hatujaanza kuwasainisha mikataba kwani kocha ameomba kupewa muda wa kumaliza ligi ili afanye chaguo kwa kuangalia wachezaji hao kama wataweza kuingia moja kwa moja kikosini,” aliongeza.
Kocha mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alieleza kuwa ndani ya timu yake msimu ujao anataka kubaki na wachezaji wenye uzoefu na ubora wa kutosha ili kutengeneza kikosi imara kitakachoshindana kimataifa.
“Yanga ni timu kubwa, inahitaji kuwa na kikosi imara ambacho kitaleta ushindani wa kutosha kwenye michuano ya kimataifa na ndani kwa msimu ujao, hivyo lazima tuhakikishe tunaendelea na wachezaji wenye ubora ndani ya kikosi ili kulitimiza hilo,” alisema.
Mwanaspoti linajua kuwa kocha Nabi alishawasisitiza viongozi wa Yanga kumalizana na mastaa wao muhimu mapema ili kuwaepusha na presha za usajili kwenda timu nyingine kwani amepanga kusajili wachezaji wasiozidi watano kutoka nje.