SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amemuonya Mbunge Sengerema, Hamisi Tabasamu (CCM) baada ya kudaiwa kutweza mchango wa Mbunge wa Momba, Condester Sichwale aliyeitaka Serikali kupima na kuzirasimisha pombe za kienyeji ikiwamo gongo ili kuwasaidia kiuchumi wanawake wanaofanya shughuli hizo.
Pia Spika Tulia amemuomba radhi Condester na kusisitiza kuwa yeye sio mbunge wa ajabu bali ni wa kawaida na ana heshima zote. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mbunge wa Momba, Condester Sichwale akitoa mchango wake bungeni huku akiwa ameshika pombe mbalimbali
Hatua hiyo imekuja baada ya mchango wa Condester katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jana tarehe 9 Mei, 2022 bungeni jijini Dodoma kuibua mtikisiko.
Condester alisema watu wanaokunywa pombe za kienyeji wanaonekana kuwa hawana akili lakini wanaokunywa bia wanaokena wa kisasa.
Alisema Shirika la Viwango Nchini (TBS), linaweza kupima wakaondoa makali yaliyoko kwenye gongo ifanane na hizo pombe ambazo matajiri wanakunywa.
Hata hivyo, baada ya mchango wa mbunge huyo ambaye alitinga na baadhi ya pombe za gongo bungeni ambazo alisema zimetoka nje ya nchi na zinauzwa hapa nchini, Mbunge Tabasamu alizungumza na waandishi wa habari nje ya bunge na ‘kuuponda’.
Mbunge Sengerema, Hamisi Tabasamu (CCM)
Akinukuliwa Tabasamu alieleza kushangazwa na mbunge mwenzie kuja kujadili suala la pombe za kienyeji ilihali sasa mjadala mkubwa ni suala la kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali ikiwamo mafuta, sukari na mikate.
“Ndio hao wabunge ambao tunasema tuna wabunge wa ajabu sana, badala ya kujadili vitu vya maana tunakuja kupotezewa muda wetu wachangiaji bungeni kujadili habari ya gongo, wakati kila kitu kimepanda bei, hii ni hatari sijawahi kuona katika nchi hii,” alisema.
Kutokana na kauli hiyo ya Tabasamu, leo tarehe 10 Mei, 2022 baada ya kipindi cha maswali na majibu Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Thea Ntara (CCM) alitoa taarifa kwa bunge kwamba Tabasamu hakutumia maneno ya kibunge bali amemdhalilisha Mbunge Condester na kiti cha Bunge.
Dk. Ntara amesema Condester alitumia uhuru wa majadiliano, alikuwa ndani ya ibara ya 11 na hakutukana, hakuvunja sheria, hakudhalilisha mtu, maelezo yake kuhusu pombe yaliungwa mkono na wabunge wenzie Dk. Kitila Mkumbo na George Simbachawene.
“Tabasamu amekiuka kanuni za Bunge kwa kuwa zinanaeleza kama mbunge hajaridhika na jambo anasimama na kuomba utaratibu, muongozo wa Spika au taarifa na kuliongea humu ndani ya bunge.
“Tabasamu hakutumia maneno ya kibunge isipokuwa ametoa kauli za kulishambua na kulidhalilisha Bunge kuhusiana nashughli zilizokuwa zinaendelea, mfano ‘wabunge wa ajabu’… ni wa ajabu kwa sababu ni mwanamke?. Amemfanya mbunge huyo kuathirika kisaikolojia,” amesema.
Kutokana na taarifa hiyo, Spika Tulia amesema maneno mahsusi aliyotumia Tabasamu nje ya Bunge sio mazuri na yanamfanya mbunge Condester asiwe na uhakika kwamba anaweza kuzungumzia nini kuhusu watu wake.
Amesema Katiba inavyolinda uhuru wa mawazo ndani ya Bunge, inaangalia ukubwa wa nchi, tofauti za jimbo moja na lingine na shughuli za wananchi wa majimbo husika.
“Nilishasema ni kazi yangu kuwalinda wabunge humu ndani na nje, kwa hiyo asitokee wa kumdhalilisha mbunge humu ndani wala nje. Hakuna mbunge wa ajabu wote wana kiapo kimoja na wote sawasawa,” amesema.
Ametolea mfano kuwa paliwahi kuwa na michango ya namna hiyo ambapo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) alichangia kuhusu bangi na Jumanne Kishimba Mbunge wa Kahama Mjini (CCM) alichangia kuhusu gongo lakini hakuna mbunge aliyewaita kuwa wabunge wa ajabu.
Mbali na kuwaomba wabunge waheshimiane, Spika Tulia angeweza kutumia kanuni mbili ya kumpeleka Tabasamu kwenye kamati ya Bunge ya maadili na kumpa onyo lakini sasa anampa onyo.
“Sasa nitoe onyo tuheshimiane, kwa sababu jambo hilo limeleta mtikisiko wa mawazo. Mimi kwa niaba ya huyo mbunge ambaye aliyefikiri wewe ni wa ajabu, nikuombe radhi.
“Wewe (Condester) si wa ajabu ni wa kawaida na una heshima zote, kama ambavyo wananchi wamekuheshimu wamekuleta humu ndani, hizo biashara ndizo zinazofanywa na wanawake huko ulikotoka.
“Kwa hiyo ni halali yako kuwatetea humu ndani, uwe na amani michango yako mingine huko baadae usijisikie vibaya kiti kinakulinda uko salama kabisa na wewe ni mheshimiwa mbunge kama wabunge wengine,” amesema Spika Dk. Tulia.