Sakata Mbatia, Msajili laingia ukurasa mpya



WAKATI Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikitangaza kubariki uamuzi wa kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, mwenyewe ameibuka na kutangaza kuwa uamuzi dhidi yake ni batili.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Mapema jana, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ilitangaza kubariki uamuzi wa kusimamishwa kwa Mbatia na sekretarieti yake yote kujihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wahabari jana mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya taarifa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mbatia alisema yeye bado ni mwenyekiti halali wa chama hicho na kikao kilichofanyika cha kumng’oa hakikuwa halali.

Mbatia alisema: "Mimi bado mwenyekiti halali wa NCCR-Mageuzi kwa mujibu wa katiba na taratibu zote za nchi, hata Katiba ya NCCR-Mageuzi. Hapa kuna ajenda fiche."

Pasi na kuweka wazi alichokiita ajenda fiche, Mbatia alisema kikao kilichofanyika kwa lengo la kumng’oa madarakani, hakikufuata taratibu, kikitumia dakika 40 kupitisha ajenda zaidi ya nne licha ya Kaimu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kubariki uamuzi wa kikao hicho.


 
“Kaimu Msajili anasema kikao kilikuwa halali, kipi hicho? Hata Makamu Mwenyekiti wangu hakuwa na taarifa, Hata Kaimu Katibu Mkuu wa chama hana taarifa. Haya yote yanayotokea ni mazingaombwe,” alisema Mbatia.

Alidai kuwa yote yanayotokea yanaongozwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini kwa akili yake anaamini hakuna wa kumnyang'anya uongozi ndani ya chama hicho.

Mbatia alisema: "Ninaloliamini kwa utu wa kibinadamu nitalisimamia. Iwe Deni la Taifa au sekta ya elimu nitalisimamia na wala sitatereka hata ikinigharimu uhai wangu, nitasimamia kwenye ukweli na ukweli utaniweka huru."


Alidai kuwa baada ya kuona taarifa katika mitandao ya kijamii jana inayotoka katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikieleza kutomtambua kama mwenyekiti wa chama hicho, aliamua kumpigia simu Kaimu Msajili wa Vyama vya Siasa, Nyahoza, lakini hukupokea simu.

Mbatia alisema alilazimika kumpigia simu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ambaye alimjibu kwamba alikuwa mjini Dodoma, hivyo asubiri hadi atakaporejea Dar es Salaam leo.

"Namheshimu Msajili wa Vyama vya Siasa. Nitamsubiri hadi kesho (leo) atakaporudi ili tuzungumze na anipe ufafanuzi. Kwa sababu nilipompigia alisema hafahamu chochote kuhusu kinachotokea sasa katika chama cha NCCR-Mageuzi, " alisema Mbatia.

MSAJILI ABARIKI

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubariki kusimamishwa kwa Mbatia na wenzake hao, kulitangazwa jana na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, akisema uamuzi wa kikao cha halmashauri ya chama hicho kilichofanyika Mei 21, mwaka huu ulikuwa halali kwa akidi ya wajumbe wake. Hata hivyo, Nyahoza hakutaja uhalali wa akidi hiyo.


 
Nyahoza alisema kwa mamlaka ya ofisi hiyo inamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapotenguliwa na chama.

“Baada ya kusimamishwa, katibu wa chama hicho alituletea barua kwa fomu ya kisheria inayotujulisha kusimamishwa uanachama, tumekubaliana na uamuzi huo. Kama hawataridhika, ziko njia za kutafuta haki, waende mahakamani," alisema Nyahoza.

Jumamosi iliyopita, Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR Mageuzi ilimsimamisha Mbatia na Makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa, kujihusisha na shughuli zozote za chama hadi mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

Mbatia na wenzake walisimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo kugombanisha viongozi na hivyo kulazimika kujiuzulu.


Hata hivyo, siku moja baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR Mageuzi kutangaza kuwasimamisha viongozi hao, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho ilikutana na kutoa maazimio manne likiwamo la kuwasimamisha nafasi za uongozi Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ambar Hamid, Mweka Hazina, Suzan Masele na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Amer Mshindan.

Akisoma maazimio hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Mohamed Tibanyendela, alisema wamewasimamisha viongozi hao hadi pale Halmashauri Kuu itakapokutana.

Tibanyendela alisema maazimio mengine ni kutotambua mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Mei 21 kutokana na kutokuwapo kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.

Pia alisema Kamati Kuu imelaani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia migogoro ya chama na tayari wameshamwandikia barua pamoja na mamlaka yake ya uteuzi.

Azimio lingine ni kutoitambua bodi ya wadhamini iliyoteuliwa kwa madai kuwa bodi hiyo iliyopo ni halali na inaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.


 
Mwenyekiti wa NCCR, Mbatia, alisema chama hicho ndicho mwasisi wa mageuzi Tanzania, hivyo wanaamini katika mwafaka wa kitaifa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad