Serikali Kununua Silaha za Raia Kuepusha Vifo Holela

Serikali ya Canada inatarajia kupitisha sheria mpya inayopiga marufuku uuzaji, ununuzi, uingizaji na uhamisho wa bunduki, sambamba na mpango wa kununua silaha zinazomilikiwa na raia wake ili kudhibiti matukio holela ya kiuhalifu nchini humo.


Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema hatua hiyo inafuatia uwepo wa matukio kadhaa ya kiuhalihu ikiwemo lile la vifo vya watu 22 waliouwawa katika kijiji cha Nova Scotia na mtu mwenye bunduki mwaka 2020.


“Kama serikali na kama jamii tuna jukumu la kuchukua hatua ili kuzuia majanga zaidi tunahitaji kujua ikiwa hatutachukua hatua kwa uthabiti na kwa haraka itakuwa mbaya zaidi na ngumu zaidi kukabiliana nayo,” amesema Trudea.


Mpango huu unaakisi ule uliochukuliwa na nchi ya New Zealand mwaka 2019 baada ya mtu aliyejihami kwa bunduki kuvamia misikiti miwili na kuuwa watu 51 na kujeruhi wengine kadhaa katika kanisa la Christchurch.


Shambulio jingine ni lile la vifo vya watu wengi nchini Australia mwaka 1996 lililoifanya Serikali ya nchi hiyo kukusanya zaidi ya bunduki 650,000 za semiautomatic na zile za aina nyingine kisha kupiga marufuku matumizi ya silaha chini ya sheria mpya.


Matumizi ya silaha kinyume na matarajio yamekuwa yakitokea katia maeneo mengi Duniani ambapo kwa nchini Tanzania novemba 2013 mfanyabiashara Gabriel Munisi (35), alijiua kwa risasi baada ya kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu jijini Dar es Salaam katika tukio lililohusishwa na wivu wa mapenzi.


Tukio hilo lilitokea ikiwa ni mwezi mmoja (Oktoba, 2013), baada ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa ITV Ufoo Saro kujeruhiwa na mama yake mzazi kuuliwa kwa risasi na mzazi mwenzake Anthery Mushi ambaye naye alijiua katika tukio lililosababishwa na masuala ya kimapenzi.


Mei 27, 2017 Maxmilian Tula (40), mkazi wa Kanyenyere kata ya Butimba jijini Mwanza alimuua mkewe Teddy Malulu kwa kumpiga risasi kisha na yeye kujiua kwa kujipiga risasi.


Aidha Mei 30, 2022 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Mairi Makori amethibitisha kifo cha mtuhumiwa Said Oswayo aliyejipiga risasi akidaiwa kumuua mkewe Swalha Salum (28), kwa kumpiga risasi kadhaa mwilini.


“Mwili huo umeopolewa ziwani eneo la ufukwe wa Rock Beach ukiwa na majeraha ya risasi kichwani na tumejiridhisha kuwa ndiye mtuhumiwa baada ya kutambuliwa na ndugu zake,” amesema Makori.


Julai 2021 Dar 24 iliripoti tukio la mwanaume mmoja Jonathan Gachunga(42), kumuua mkewe na kisha baadaye kujipiga risasi kichwani nyumbani kwao Kaunti ya Kiambu nchini Kenya.


Mamlaka stahiki zinapaswa kukemea kisha kuchukua hatua zitakazoondosha matukio ya vifo vinayosababishwa na matumizi ya silaha kwani yanaacha maumivu na majonzi kwa baadhi ya familia na kuharibu mustakabali wa maisha yao

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad