Serikali yafufua Majadiliano MRADI Bandari ya Bagamoyo



SERIKALI imefufua majadiliano na wawekezaji watakaoendeleza Mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Kiuchumi Bagamoyo.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alibainisha hayo jana bungeni alipowasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake mwaka wa fedha 2022/23, akiliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 99.1.

Dk. Kijaji alisema wizara inaratibu uendelezaji wa Mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Kiuchumi Bagamoyo unaolenga kuwezesha nchi kuendana na ushindani wa biashara za usafiri wa majini na muunganisho na shughuli nyingine za kiuchumi ikiwamo viwanda na utalii.

Dk. Kijaji alisema: “Wizara imefufua majadiliano na wawekezaji wa Kampuni za China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Oman Investment Authority (OIA) ambayo awali ilikuwa inaitwa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (State General Reserve Fund – SGRF).

“Majadiliano hayo yanahusu eneo dogo la Mradi wa BSEZ kwa kuendeleza eneo la hekta 3,087 kati ya hekta 9,887, unahusisha ujenzi wa bandari na Kituo cha Usafirishaji (Logistics Park) kwenye eneo la hekta 887 na uendelezaji wa eneo maalum la viwanda (Portside Industrial City) kwenye eneo la hekta 2,200.”


Alisema msingi wa marejeo ya majadiliano hayo ambayo yalisimama mwaka 2018 ni kuhakikisha kuwa serikali inatekeleza maeneo ambayo ni wajibu wake kama vile ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, reli, umeme, maji, gesi na mifumo ya mawasiliano) na lango la kuingilia bandarini kwa maslahi mapana ya Taifa.

Dk. Kijaji alisema uwekezaji katika maeneo ya mradi utafanywa kwa kuvutia wabia wa sekta ya umma na sekta binafsi au kufanywa na mwekezaji binafsi.

Kuhusu vipaumbele vya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23, Dk. Kijaji alivitaja kuwa ni kutekeleza miradi ya kipaumbele iliyoko katika mipango na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.


Alitaja kipaumbele kingine ni uwekezaji katika kongani na maendelezo kwenye SEZ, EPZA, kongani za viwanda mfano - kongani ya kigamboni, Kwala na Kitaraka.

Kingine ni usimamizi na udhibiti wa masoko, ushiriki katika shughuli za kikanda -- Jumuiya ya Afrika Masharki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), AfCFTA na kimataifa.

Dk. Kijaji alisema kipaumbele kingine ni kuondoa urasimu katika kuhudumia wawekezaji na wafanyabiashara, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi moja kwa moja katika uchumi na uwezeshaji wa wananchi.

Waziri huyo alitaja vipaumbele mahususi ambavyo ni kuendelea kuratibu programu za uhamasishaji wa uwekezaji ndani na nje ya nchi, kuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na maendeleo ya sekta binafsi.

Kingine ni kuratibu ufanikishaji wa uwekezaji ikiwamo kuongeza ufanisi wa miradi ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Kingine ni kuratibu uanzishaji na uendelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji yenye manufaa mapana kwa Taifa, kuimarisha mifumo ya kushughulikia kero za uwekezaji.

Alitaja kingine ni kuboresha mazingira wezeshi ya kuendeleza viwanda na biashara kwa kupitia na kutunga sheria, sera na mikakati ya kuvutia uwekezaji.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad