WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa washirika wa maendeleo kuchangia kwa hali na mali kiasi cha dola za Marekani milioni 80 kwa ajili ya kufanikisha sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Dk Nchemba alitoa wito huo jijini Dar es Salaam alipofungua mkutano wa washirika wa maendeleo wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Alisema kuwa sensa ya watu na makazi imekadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 272.7 sawa na Sh bilioni 626.9 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 na kati ya fedha hizo serikali itachangia asilimia 70 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 81.8 kitachangiwa na washirika wa maendeleo.
Dk Nchemba alisema kuwa sensa ya watu na makazi inatumia rasilimali kubwa ndiyo maana serikali imeamua kuwashirikisha kikamilifu wadau wa maendeleo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa siku ya sensa itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.
“Sensa ni muhimu kwa wananchi wote kwa sababu imebainika kuwa wakati wa sensa watu hawajitokezi lakini wanapodai kujengewa miundombinu kama elimu, afya na kutaka maeneo yao kupandishwa hadhi wanajitokeza kwa wingi, lakini tukirudi kwenye takwimu tunakuta idadi ya wananchi wachache,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk Khalid Salum Mohamed, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango, Zanzibar Dk Saada Mkuya Salum, aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa kutoa ahadi zao za kusaidia sensa na kuwaomba watimize ahadi hizo kwani muda uliobaki ni mfupi.
Mabalozi na wakuu wa mashirika ya Kimataifa walioshiriki mkutano huo wameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maandalizi ya sensa kwa kutumia fedha zake za ndani na kutoka kwa baadhi ya mashirika ya kimataifa na kuahidi kuwa watachangia vifaa na fedha ili kusaidia kazi hiyo.
Kwa upande wa Benki ya Dunia imeahidi kutoa dola za Marekani milioni 19 kwa ajili ya kuchangia sensa, aidha Shirika la Umoja wa Mataifa (UNWomen) limeahidi kuchangia vishikwambi 200 huku mataifa mengine yakiendelea kutoa ahadi za kufanikisha sensa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya Idadi ya Watu na Makazi Mark Shreiner, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Spika Mstaafu Anne Makinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma na Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohammed Haji Hamza.