Dar es Salaam. Mwanazuoni mkongwe nchini, Profesa Issa Shivji amesema sehemu kubwa ya wasomi nchini wameshindwa kulisaidia Taifa kwa kutoa ushauri unaofaa huku wakisubiri kuteuliwa kwenye nyadhifa mbalimbali.
Profesa Shivji, gwiji la sheria kitaifa na kimataifa alitoa kauli hiyo juzi, katika mahojiano ya kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na ITV ambapo pia alizungumzia miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere.
“Mimi ni msomi, nakiri sitaki kusema nipo tofauti na wengine, zamani wasomi walikuwa wanakosoa na kushauri, tuliandika, tulikuwa na midahalo, tunazungumza, lakini sasa hivi hatusikii. Kulikuwa na wakati wasomi walikuwa wanajipanga katika foleni ya kusubiri kuteuliwa, sasa kama una matumaini ya kuteuliwa hutakosoa wala kuzungumza mambo.
“Ingawa kulikuwa na hofu pia na hilo linaeleweka pia, lakini kwa kiasi gani wasomi tumetekeleza jukumu letu. Hivi sasa wamepumua kidogo na wanaweza kuanza upya kutekeleza majukumu yao,” alisema Profesa Shivji.
Profesa Shivji alisema kunahitajika kazi ya ziada kukosoa wazo tawala na kutoa mbadala wake ili kuleta mabadiliko katika jamii ambapo alisema kazi mojawapo ya wasomi au wanazuoni ni kukosoa na kutoa wazo mbadala.
“Hatua hii itasaidia wananchi kuona kwamba kuna njia nyingine za kufanya mambo, kuelewa ukweli na kuangalia hali halisi, sio tunayoambiwa siku zote. Lazima nikiri ni jukumu letu, lakini wasomi tumefeli sana katika jukumu hili hasa katika miongo miwili iliyopita.
“Wananchi wakitulaumu tunastahili kulaumiwa kwa kweli, lakini lazima tujikumbushe haikuwa hivyo Tanzania. Wasomi au wanazuoni wa nje hadi leo wanakumbuka wasomi wa Tanzania, walichoandika, walichojadili na walichopendekeza hadi leo wanatukumbuka,” alisema.
Profesa Shivji alisema bado wasomi wa nje wanashangaa na kuhoji nini kilichotokea kwa wasomi wa Tanzania.
Hata hivyo, msomi huyo alisema wananchi wana uwezo wa kukosoa wazo tawala, akisema mara nyingine ukizungumza nao unajifunza masuala mengi kutoka kwao, ingawa wanavyozungumza sio kama wasomi.
Kwa mujibu wa Profesa Shivji, wasomi walikuwa wanafanya hivyo miaka ya 70 hadi 80 wasomi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na pale ilipohitaji walikuwa wanaikosoa Serikali.
“Baadhi ya wasomi wetu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hatukukubaliana moja kwa moja na Mwalimu (Nyerere) kuhusu sera za kilimo. Hata wakati wa Nyerere hatukuweza kuleta mapinduzi ya kilimo, tulifuata nyayo za kikoloni,” alisema.
Kauli ya Profesa Shivji imeungwa mkono na Mwenyekiti Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), Dk Aviti Mushi aliyesema miaka kadhaa wasomi walikuwa na hofu ya kukosoa masuala mbalimbali.
“Wale waliojitokeza kukosoa waliitwa majina mabaya mara sio wazalendo au vibaraka, hali hii ilisababisha wasomi kutotoa maoni, huku wengine wakifunga mdomo na kutafuta ugali wao. Walioonekana kimya ndio walikuwa bora na kupata nafasi za uteuzi katika maeneo mbalimbali,” alisema Dk Mushi alipozungumza na Mwananchi kwa simu jana.
Aliendelea kusema kuwa, kauli ya Profesa Shivji ina uhalisia kutokana na hali iliyopo na kwamba ilifika wakati wasomi walikuwa wana hofu kuzungumza na vyombo vya habari ili kutoa maoni yao wakihofia kuitwa majina mabaya. “Wasomi tulijikuta hatuwezi kuzungumza na vyombo vya habari, hasa kutoa maoni yanayokinzana na Serikali. Ingawa sasa hivi kuna mabadiliko yametokea,” alisema.