SIMBA SC ipo katika mipango ya kumrejesha kikosini kwao kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya ambaye hivi sasa anakipiga Namungo FC.
Hiyo ni katika kuhakikisha wanaimarisha kikosi chao maeneo yote muhimu kuelekea msimu ujao wa 2022/23.
Kichuya mara ya kwanza alijiunga na Simba Julai 2016 akitokea Mtibwa Sugar ambapo alicheza hapo hadi Januari 2019 alipotimkia Misri kujiunga na Pharco FC, kisha Enppi SC, kabla ya kurudi Simba Januari 15, 2020. Mwisho wa msimu wa 2020/21, akajiunga na Namungo alipo hadi sasa.
Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, wamepanga kuwaacha wachezaji wanne wazawa na kuwasajili wengine wapya kwa idadi hiyo.
Bosi huyo alisema katika wachezaji wapya wazawa watakaosajiliwa kikosini hapo, mpaka sasa jina la Kichuya lipo mezani kwao ambapo mazungumzo ya awali yameanza kati ya kiungo huyo na uongozi wa Simba.
“Kichuya ameonekana kubadilika tangu ajiunge na Namungo kutokana kiwango chake kile bora kurejea.
“Upo uwezekano mkubwa wa Kichuya kurejea Simba kutokana na ubora wake huo, kwani uongozi umepanga kusajili wachezaji wanne wazawa na kati ya hao jina lake lipo.
“Kichuya ana uzoefu wa kucheza popote pale iwe kiwanja kigumu au kizuri, hiyo itatusaidia katika ligi ambayo inachezwa katika viwanja vya namna hiyo,” alisema bosi huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alizungumzia hilo la usajili akisema: “Wapo wachezaji wengi ambao kocha Pablo (Franco) amewapendekeza wasajiliwe baada ya kuona viwango vyao, hivi sasa hatutawaweka wazi hadi hapo baadaye.”
Msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Kichuya amehusika kwenye mabao matano kati ya 28 yaliyofungwa na Namungo, amefunga matatu na kutoa asisti mbili.
STORI: WILBERT MOLANDI